1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wakubaliwa kuingia Syria

MjahidA15 Agosti 2013

Umoja wa Mataifa umesema wakaguzi wa silaha za kemikali wanatarajiwa kwenda nchini Syria baada ya nchi hiyo kukubali ujio wa wakaguzi hao.

Khan al-Assal
Khan al-AssalPicha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa yake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema Syria imekubali waangalizi hao kuingia nchini humo kufanya uchunguzi juu ya matumizi ya silaha za kemikali zilizodaiwa kutumika dhidi ya waandamanaji.

Kundi hilo la waangalizi 10 litakaloongozwa na mtaalamu wa maswala ya silaha raia wa Sweden, Ake Sellstroem, watakaa nchini Syria kwa muda wa wiki mbili wakitembelea na kukagua maeneo ambayo silaha hizo zinadaiwa kutumika.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.Picha: Reuters

Wakaguzi hao wa Umoja wa Mataifa awali walinyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo baada ya kutokea mkwaruzano kati yake na rais Bashar Al Assad juu ya namna watakavyoendesha uchunguzi huo.

Hata hivyo mwezi uliopita Umoja wa Mataifa walifikia maelewano na serikali ya Syria kuingia nchini humo na kufanya ukaguzi lakini wakawa wanasubiri tu fursa kutoka kwa serikali ya Syria iliyokubali ushirikiano na Umoja huo ili kuhakikisha utekelezaji mzuri, salama na wenyewe uhakika wa ujumbe huo.

Maeneo yatakayofanyiwa uchunguzi

Moja ya eneo ambalo litafanyiwa uchunguzi ni Khan al-Assal lililo karibu na mji wa Aleppo mahali ambapo serikali inadai waasi walitumia silaha za kemikali katika ghasia za Machi 19 ambapo watu 26 waliuwawa wakiwemo wanajeshi 16 wa serikali.

Hata baada ya wakaguzi hao kupewa nafasi ya kuingia nchini humo wameekewa masharti kuwa uchunguzi wao waufanye tu katika eneo la Khan Al Assal. Wakaguzi hao pia wataangalia iwapo silaha za kemikali zimetumika na kama ndio watakuwa na jukumu la kuelezea pia ni za aina gani.

Mtaalamu wa maswala ya silaha raia wa Sweden, Ake SellstroemPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa bado hawajasema wazi ni maeneo gani mengine kando na Khan Al Assal watakayoyachunguza, lakini wamesema ripoti yao haitaegemea upande wowote. Kufuatia jamii ya kimataifa kutoa uungwaji mkono mkubwa kwa wakaguzi kufanya kazi yao hii inadhihirisha wazi kuwa wale watakaopatikana na makosa ya kutumia silaha hizo bila shaka watakuwa wametenda uhalifu mkubwa.

Kwa upande wa upinzani nchini Syria wamesema kuwa wakaguzi hao watakuwa na nafasi ya kuingia katika maeneo wanayoyadhibiti ili kufanya uchunguzi wao.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo