Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wawasili Zaporizhzhia
1 Septemba 2022Ziara ya timu ya watu 14 inayoongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi inafanyika wakati ambapo kinu hicho kikubwa cha nishati ya nyuklia barani Ulaya kikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo Urusi na Ukraine zimekuwa zikishutumiana kuyafanya.
Timu hiyo itatathmini hatari inayoweza kutokea kutokana na kuvuja kwa mionzi katika kinu hicho, baada ya kucheleweshwa kwa saa kadhaa kutokana na mashambulizi ya makombora karibu na kinu hicho kinachodhobitiwa na Urusi.
Shirika la Habari la Reuters limeshuhudia ujumbe wa IAEA ukiwasili majira ya saa tisa alasiri na msafara mkubwa, huku wanajeshi wengi wa Urusi wakiwa karibu. Duru za Ukraine zimeeleza kuwa ziara ya ujumbe huo inaweza kuwa fupi kuliko ilivyopangwa awali.
Urusi kuhakikisha usalama Zaporizhzhia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema nchi yake inafanya kila linalowezakana kuhakikisha kinu hicho kinaendeshwa kwa kuzingatia usalama na kwamba wakaguzi wa IAEA watafanikiwa kukamilisha majukumu yao.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema Ukraine itawajibika kutokana na majaribio kadhaa ya hujuma na mashambulizi na madhara yake yatauangukia utawala wa Rais Volodymyr Zelensky na kundi lake la nchi za Magharibi ambalo linamuunga mkono.
Nayo wizara ya ulinzi ya Urusi imesema Alhamisi kuwa hali katika kinu cha Zaporizhzhia ni ngumu, lakini inaendelea kudhibitiwa, baada ya kuwepo taarifaza mashambulizi karibu na mji wa Enerhodar.
Dmitry Peskov, msemaji wa Rais wa Urusi Vladmir Putin, amesema bila masharti wanaogopa uchokozi kutoka upande wa Ukraine. "Kwa kuzingatia kwamba mashambulizi ya kikatili na ya uchochezi hayaishi, tunaweza kuona majaribio ya kudhoofisha usalama. BAdo tuko tayari kuwasiliana na ujumbe wa IAEA unaokitemblea kinu hiki cha kuzalishia umeme," alifafanua Peskov.
Ama kwa upande mwingine, gavana aliyewekwa na Urusi katika wilaya ya Zaporizhzhia, Yevgeny Balitsky amesema takribani watu watatu wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa katika kile alichosema mashambulizi ya makombora ya Ukraine katika eneo la Enerhodar.
Balitsky amesema shambulizi hilo limeharibu pia shule tatu za chekechea na nyumba ya makumbusho. Umeme katika mji huo umekwatwa tangu asubuhi.
HRW: Vikosi vya Urusi viliwahamisha raia kwa lazima
Wakati huo huo, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Human Rights Watch, limesema kuwa vikosi vya Urusi viliwahamisha kwa lazima raia wa Ukraine, ikiwemo wale wanaokimbia mapigano na kuwapeleka kwenye maeneo wanayoyadhibiti.
Shirika hilo limesema uhamisho wa lazima ni ukiukaji mkubwa wa sheria za vita unaoweza kusababisha mashtaka ya uhalifu wa kivita na uwezakano wa uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Huku hayo yakijiri, Ikulu ya Urusi, Kremlin imeukosoa uamuzi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kusitisha makubaliano ya mwaka 2007 ya kurahisisha utoaji wa visa na Urusi kutokana na mzozo wa Ukraine na imeonya kuhusu hatua inazoweza kuchukua.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari siku ya Alhamisi kwamba uamuzi huo ni mbaya kwa wananchi wa Urusi, lakini utakuwa mbaya zaidi kwa raia wa Ulaya pia.
Aidha, Umoja wa Ulaya unaanzisha kituo karibu na mpaka wa Poland na Ukraine kwa ajili ya watu wanaokimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambapo wataweza kuchunguzwa afya zao na kupelekwa kwenye vituo vya matibabu vya Ulaya haraka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi na Halmashauri Kuu ya Ulaya, kituo hicho kitaanzishwa kwenye mji wa Rzeszow, ambacho hakiko tu karibu na mpaka wa Ukraine, bali pia karibu na uwanja wa ndege.
(AFP, DPA, AP, Reuters)