Wakala wa kandanda akasirishwa na ripoti za kifo chake
28 Aprili 2022Taarifa kuhusiana na kifo cha Raiola ambaye ni wakala wa wachezaji Paul Pogba wa Manchester United na mshambuliaji mahiri chipukizi Erling Braut Haaland, zilienea kwa haraka Alhamis kote duniani kutoka nchini Italia.
Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa uvumi kama huo kukanushwa na Raiola na ujumbe wake.
"Hali yangu ya afya kwa sasa kwa wale wanaoshangaa: nimeghadhabishwa na wale walioniua kwa mara ya pili katika miezi minne. Inaonekana wanaweza kumfufua mtu pia," ulisoma ujumbe ulioandikwa katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa Raiola.
Gazeti la Gazzetta Dello Sport ambalo ndilo gazeti kuu la kila siku la michezo nchini Italia lilikuwa hata limechapisha ujumbe wa tanzia wa Raiola ambaye alizaliwa kusini mwa Italia.
Wakala wa Raiola alipoulizwa na shirika la habari la Ufaransa AFP, amesema, habari hizo ni za uongo na kwamba Raiola hajafariki.
Raiola apigania maisha yake chumba cha wagonjwa mahututi
Shirika la habari la Italia ANSA limemnukuu Alberto Zangrillo, mkuu wa kitengo cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya San Raffaele kidogo tu ya mji wa Milan, akisema Raiola yuko hali mbaya na anapigania maisha yake kwa sasa.
"Ninaghadhabishwa kupokea simu kutoka kwa waandishi ambao wanaeneza uvumi kuhusiana na mtu anayepigania maisha yake kwa sasa," alisema Zangrillo.
Raiola ambaye mshambuliaji wa AC Milan Zlatan Ibrahimovic pia ni mteja wake, ni mmoja wa mawakala wenye ushawishi mkubwa mno katika michezo na pia ni wakala mwenye utata mno.
Ametuhumiwa kwa kuongeza pakubwa mishahara ya wachezaji wakati wa majadiliano na pia amehusishwa na utata mwingi kuhusiana na ada za wakala wakati wa uhamisho wa wachezaji.
Mwaka 2016, Raiola aliripotiwa kulipwa dola milioni 28.3 kutokana na kumuuza Paul Pogba kutoka Juventus kuelekea Manchester United.
Chanzo: AFPE/DPAE