Wakatalani wapiga kura kutaka kujitenga na Uhispania
1 Oktoba 2017Polisi walivunja milango kwa nguvu na kuingia katika vituo vya kupigia kura wakati wakatalani ambao wameonesha ukaidi wakipiga kelele "majeshi ya uvamizi yaondoke!" na kuimba wimbo wa taifa wa jimbo hilo tajiri la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Katika tukio moja mjini Barcelona, polisi walifyatua risasi za mipira.
Kura hiyo ya maoni , iliyotangazwa kuwa ni kinyume na sheria na serikali kuu mjini Madrid, imeiweka nchi hiyo katika mzozo mkubwa kabisa wa kikatiba katika muda wa miongo kadhaa na kusababisha kujitokeza zaidi mtengano wa karne nyingi kati ya Madrid na Barcelona.
Licha ya hatua hizo za polisi, mamia ya watu walijitokeza katika milolongo mirefu katika miji na vijiji katika jimbo hilo kupiga kura zao. Katika kituo kimoja cha kupigia kura mjini Barcelona, watu wazima na wanawake wenye watoto waliingia kwanza.
"Nina furaha kubwa kwasababu licha ya vikwazo vyote vilivyowekwa, nimefanikiwa kupiga kura," amesema Teresa , mstaafu mwenye umri wa miaka 72 mjini Barcelona ambaye alisimama katika msitari kwa masaa sita.
Kura hiyo haitakuwa na uhalali wa kisheria kwa kuwa imepigwa marufuku na mahakama ya katiba ya Uhispania , na serikali kuu mjini Madrid kwa kukiuka katiba ya mwaka 1978.
Wachache wapendelea kujitenga
Idadi ndogo ya watu kiasi ya asilimia 40 ya Wakatalani wanaunga mkono kura ya maoni, uchunguzi wa maoni ya wapiga kura unaonesha, licha ya kuwa idadi kubwa ya watu wanataka kura hiyo ya maoni ifanyike kuhusiana na suala hilo. Jimbo hilo lenye wakaazi milioni 7.5 lina uchumi mkubwa kuliko ule wa Ureno.
Polisi 11 tisa kutoka jeshi la taifa la polisi na wawili kutoka katika kikosi cha ulinzi wa umma wamejeruhiwa wakati wakijaribu kuzuwia kura hiyo ya maoni iliyopigwa marufuku katika jimbo la Catalonia.
Pia baadhi ya walinzi hao wa umma , "wakiponyoka haraka" wakikimbia na gari yao kutoka katika kundi la watu waliokuwa wakiirushia mawe gari hiyo katika eneo la Saint Carles de la Rapita, kiasi ya kilometa 180 kusini magharibi mwa Barcelona.
Wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania imetoa taarifa hizo kupitia mtandao wa Twitter, baada ya maafisa wa afya jimboni Catalonia kusema wapiga kura 38 wamejeruhiwa kufuatia mapambano na "polisi wa Uhispania," ikiwa ni pamoja na tisa ambao wamepelekwa hospitali.
Mbunge wa bunge la Israel anayeangalia kura hiyo ya maoni ya kudai uhuru jimboni Catalonia amesema ameshitushwa na polisi wa Uhispania kutumia risasi za mipira dhidi ya makundi ya watu ambao hawana silaha. Ksenia svetlova amesema leo Jumapili (01.10.2017) kwamba risasi zilizotumika "zinaweza kuvunjavunja kichwa cha mtu," amesema hakutarajia kuona mbinu kama hizo barani Ulaya.Amesema ameona watu wakivuja damu na waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Hamidou , Oummilkheir