1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakati kwa Macron kuanza kazi

Admin.WagnerD8 Mei 2017

Katika shughuli zake za kwanza rasmi baada ya kushinda uchaguzi wa rais Emmanuel Macron ameungana na Rais Fracois Hollande anayemaliza muda wake kuweka shada la mauwa katika kaburi la askari asiyejulikana mjini Paris .

Frankreich Emmanuel Macron
Picha: Reuters/F. Mori

Viongozi hao wawili walisimama bega kwa bega wakati bendi ikipiga wimbo wa taifa wa Ufaransa wa "Marseillaise" na wimbo unaohusiana na wakaazi wa Paris waliopambana na vikosi vya Ujerumani viliokuwa vikiikalia kwa mabavu Ufaransa leo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 72 ya ushindi wa majeshi ya muungano katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Hollande alimkaribishwa Macron kwa heshima wakati sherehe za maadhimisho zilipoanza huku mrithi wake huyo ambaye alishambuliwa na wapinzani wake wakati wa kampeni kuwa ni mrithi wa rais msoshalisti aliyepoteza umaarufu akitabasamu.

Hollande amethibitisha kwamba makabidhiano rasmi ya madaraka yatafanyika Jumapili.

Hollande tayari kumshauri Macron

Rais mteule Emmanuel Macron na Rais Francois Hollande anayemaliza muda wake.Picha: Reuters/S. De Sakutin

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya hapo Hollande amesema iwapo Macron atakuwa anahitaji msaada wakati wowote ule,taarifa yoyote ile,ushauri wowote ule, au uzoefu daima atakuwepo kwa ajili yake.

Alipoulizwa iwapo Macron ni mrithi wake Hollande alijibu : "Sitaki kummiliki Emmanuel Macron ni wananchi wa Ufaransa waliomchaguwa.Ni kweli alikuwa akinifuata miaka hii ya mwisho wakati mimi mwenye nikiwa mgombea na nilipokuwa rais alikuwa waziri katika serikali lakini baada ya hapo alikuwa huru na kutaka kuwasilisha mpango wake kwa wananchi wa Ufaransa, amewajisilisha mbele yao, amechaguliwa na yeye ni rais."

Alipoulizwa iwapo amemsaliti Hollande amesema hapana amekifanya kile alichoona inabidi afanye amesema amefanya hivyo akiwa upande wake na baadae akiwa peke yake na hivi sasa akiwa na wananchi wa Ufaransa amempongeza kwa ushindi huo.

Ushindi wa Macron wabeba matumaini ya mamilioni

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema amefurahishwa na ushindi huo wa Macron unaobeba matumaini ya mamlioni ya watu. Merkel amesema "Emmanuel Macron anabeba matumaini ya mamlioni ya wananchi wa Ufaransa halikadhalika ya Wajerumani wengi na barani kote Ulaya.Ameongoza kampeni ya ujasiri ya kuunga mkono Umoja wa Ulaya amesimama kutetea tamaduni tafauti, amepigania uchumi wa soko huria na tunanajuwa kwamba Ufaransa na Ujerumani zimeuganishwa kwa majaaliwa."

Mshirika wa karibu wa Macron amesema rais huyo mpya ziara yake ya kwanza itakuwa nchini Ujerumani baada ya kuapishwa.Hata hivyo pia inasemekana kwamba ziara yake ya kwanza itakuwa ni kuvitembelea vikosi vya Ufaransa vinavyotumika nchi za nje.

Macron akiwa na umri wa miaka 39 anakuwa rais kijana kabisa kushika wadhifa wa urais katika historia ya Ufaransa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri :Josephat Charo