1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakatoliki wautazama kwa siku ya mwisho mwili wa Benedict

4 Januari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amempongeza marehemu Papa Benedict XVI alipokuwa akiuongoza umati Vatican huku maelfu wakitoa heshima zao za mwisho katika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter.

Vatikan Aufbahrung Papst Benedikt
Picha: Vatican Media via REUTERS

Papa Francis amepokelewa kwa vifijo na umati wa watu uliokuwa katika ukumbi wa Paul wa sita, waliokuwa wakimtakia maisha marefu, wakati alipokuwa akiwasili kwa katekisi yake ya kila wiki na waumini wa Kikatoliki.

Haya yamefanyika wakati ambapo makumi kwa maelfu ya watu wakiwa bado wanaendelea kumiminika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter kutoa heshima zao mbele ya mwili wa papa Benedict ambao umelala kanisani humo.

Papa Francis kuongoza mazishi ya Benedict

Siku mbili za kwanza za kuutazama mwili huo zilivutia jumla ya watu 135,000. Shughuli ya Jumatano ya kuutazama mwili huo imeanza kabla alfajiri na inatarajiwa kuisha baadae Jumatano jioni.

Kiomngozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Papa Francis ndiye atakayeongoza mazishi ya Benedict hapo Alhamis, hafla ambayo itahudhuriwa na viongozi wa mataifa mbalimbali licha ya juhudi za Vatican za kutaka mazishi hayo ya kwanza ya papa katika miaka ya sasa kutowavutia wengi.

"Ningependa tuungane na wale ambao wanatoa heshima zao za mwisho wa Papa Benedict wa kumi na sita na nitoe maoni yangu kumhusu. Alikuwa ameshika dini mno, alikuwa hana ubinafsi katika fikra ila alikuwa analifikiria kanisa tu kwasababu alikuwa anataka kuandamana nasi katika kukutana na Yesu," alisema Papa Francis.

Baadae Jumatano, maafisa wa Vatican watauweka mwili wa papa Benedict katika jeneza la kwanza kati ya matatu, pamoja na historia fupi ya maisha yake ya upapa.

Baadae, mwili wa papa huyo aliyestaafu utarudishwa kanisani ambapo utahamishwa katika jeneza la pili na kisha mwishowe kutiwa katika jeneza la tatu.

Benedict alichaguliwa kuwa papa 2005

Hatimaye kama alivyotaka mwenyewe, mwili wa papa Benedict utawekwa katika chumba kilicho chini ya ardhi katika Kanisa hilo kuu, ambacho wakati mmoja kilikuwa na mwili wa aliyekuwa papa Mtakatifu John Paul wa Pili.

Waumini wa Kikatoliki wakiwa kwenye foleni kuelekea kuuona mwili wa Papa Benedict katika Kanisa Kuu la Mtakatifu PeterPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Benedict ambaye alichaguliwa kuwa papa mwaka 2005 kufuatia kifo cha John Paul wa pili, alikuwa papa wa kwanza kujiuzulu alipotoa tangazo hilo mwaka 2013 akisema hana nguvu tena za kuliongoza Kanisa Katoliki.

Baada ya Papa Francis kuchaguliwa, papa Benedict aliishi katika eneo lililobadilishwa na kuwa nyumba ya watawa huko Vatican katika muda wake wote aliostaafu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW