Wakazi wa Akobo, Sudan Kusini wako hatarini kushambuliwa
10 Machi 2026
MSF limesema waliondoka Akobo Jumamosi na vifaa vilivyokuwa kwenye ofisi zao viliibwa, siku moja baada ya jeshi kuyaagiza mashirika ya kigeni kuondoka. Taarifa ya shirika hili imeongeza kuwa wakazi wa Akobo kwa sasa wamebakiwa na machaguo mawili tu, ya ama kukimbia bila ya ulinzi wowote au kubakia na kuendelea kuishi na wasiwasi wa kuuawa.
Mkuu wa ujumbe wa MSF nchini humo Christophe Garnier amesema watu wa eneo hilo wanaathirika sana na familia zinalazimika kuyakimbia makazi yao mara kwa mara, licha ya kutokuwa na mahali salama pa kwenda. Akasema kuondoka kwao pia kumewaacha watu wa eneo hilo bila ya huduma za kutosha za tiba.
"Tunawazungumzia maelfu ya wakimbizi wa ndani. Wamechoka sana, Hawapati huduma za afya wala maji. Mzozo huu kwa mara nyingine utawaongezea madhila. Timu zetu zimeanza kujiandaa na huduma za dharura kuwasaidia wakimbizi wa ndani, kuanzia kiafya, chanjo lakini pia kuwaandaa na msimu wa malaria utakaoanza hivi karibuni."
Umoja wa Mataifa wagomea agizo hilo
Hata hivyo Umoja wa Mataifa umeliambia shirika la habari la AFP kwamba halikukubaliana na agizo hilo. Msemaji wa Ujumbe wake nchini Sudan Kusini Priyanka Chowdhury amesema walinda amani wa umoja huo wataendelea kubakia kwenye mji wa Akobo na kuendeleza majukumu yao.
Eneo la Jonglei umekuwa kitovu cha mapigano kati ya serikali na vikosi vya upinzani tangu mwezi Disemba na kusababisha karibu watu 280,000 kuyakimbia makazi yao, wakati makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu Riek Machar yakivunjika.
AFP ilitembelea hospitali ya Akobo mwezi uliopita na kuikuta katika hali mbaya sana, kuanzia majengo yasiyokuwa na milango ama madirisha hadi daktari mmoja tu wa upasuaji aliyeonekana kuelemewa sana. Kulingana na MSF, majengo yake nchini humo pia yalishambuliwa mara 12 mwaka uliopita, hatua iliyowalazimu kufunga hospitali zao tatu.
Sudan Kusini haijawa na utulivu mkubwa tangu ilipopata uhuru
Msemaji wa jeshi la serikali Lul Ruai Koang ameliambia shirika la AFP kwamba wananuia kufanya operesheni za kijeshi kwenye mji wa Akobo na maeneo yanayouzunguka, huku akivitupia lawama vikosi vya upinzani kwa kupora kwenye hospitali, na kuongeza kuwa kwa kuwa muda ilioutoa wa masaa 72 umekwishapita, sasa ni jukumu la makamanda wanaoongoza vikosi vyao kuamua hatua inayofuata.
Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwaka 2011, lakini muda mfupi baadae ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikosi vya Kiir na Machar. Makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa mwaka 2018 yalirejesha amani kwa muda, lakini yalivunjika mwaka uliopita.