1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakazi wa Mombasa watekeleza haki yao kikatiba

9 Agosti 2022

Siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu hatimaye imewadia, maelfu ya Wakenya kutoka Mombasa wamejitokeza kwa wingi mapema Jumanne katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kuwachagua viongozi wao.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Wakenya kutoka Mombasa wamejitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vya kupigia kura na kupanga foleni ndefu ili waweze kupiga kura.

Hata hivyo, kumekuwa na vurumai katika kituo cha kupigia kura cha Tudor, Mombasa ambapo afisa wa polisi aliyekuwa anatuliza hali amejeruhiwa na baadhi ya watu kutiwa mbaroni.

Aidha, kwenye baadhi ya vituo vya kupiga kura maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC wamekuwa na changamoto ya mitambo na pia baadhi ya masanduku ya kupiga kura hayakuwa na nambari za usajili, hali iliyowafanya wananchi kulalamika kukosa mwelekeo na huduma duni kutoka IEBC.

Baadhi ya wagombea wakamatwa

Anayewania kiti cha ubunge katika jimbo la Mvita Omar Shallo na anayewania kiti cha uwakilishi wa Wadi Samir Bhallo wamekamatwa na maafisa wa polisi na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Makupa baada ya vurumai kuzuka katika kituo hicho, hali iliyosababisha afisa wa polisi kujeruhiwa.

Msimamizi wa uchaguzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Swalha Yusuf amewataka wakaazi wa Mombasa kuwa watulivu na maafisa wa IEBC kuendelea kufanya kazi kuwasaidia Wakenya waweze kufanikiwa kupiga kura.

Kwengineko katika kituo cha kupigia kura cha Mwamwei kaunti ya Kwale kumekuwa na tuhuma za watu kuwapa hongo wenyeji ili waende wakawapigie kura baadhi ya viongozi. Maafisa wa polisi wanalishughulikia suala hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW