1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakazi waliokoseshwa makao Syria wazuiliwa kurejea nyumbani

16 Oktoba 2018

Syria inawazuia wakaazi waliokoseshwa makao kutoka katika maeneo yaliyokuwa yakishiliwa na watu walioipinga serikali, dhidi ya kurejea katika ardhi yao, kwa mujibu wa Shirika la Huma Rights Watch.

Syrien Evakuierung in Darayya einem Vorort von Damaskus
Picha: Reuters/Sana

Wakazi wa mji wa Qaboun wanasema serikali pia inabomoa mali yao bila ilani, na bila kuwapa makao mbadala au hata fidia. Shirika la Human Rights watch limechambua picha za satelaiti za mitaa ya Qaboun ambazo zimeonesha ubomoaji mkubwa ulioanza mwishoni mwa mwezi Mei mwaka wa 2017 baada ya mapigano kuisha eneo hilo. Picha hizo zimethibitisha kuwa bado ubomoaji unaendelea.

Mkurugenzi msaidizi wa Shirika la Huma Rights Watch eneo la Mashariki ya Kati Lama Fakih amesema Urusi na Syria inawaita watu kurejea kupewa ufadhili wa kujenga makazi yao upya lakini kama kawaida kwa serikali ya Syria, uhalisia ni tofauti. Mwezi Aprili mwaka huu, Baraza la mawaziri la Syria na idara husika zilitenga maeneo ya mji wa Darayya kwa ujenzi upya wa makazi kufanywa na mwezi Julai wakatenga maeneo katika mji wa Qaboun.

Picha: Reuters/Sana

Serikali ya Syria iliichukua miji hiyo baada ya mashambulizi makubwa kutekelezwa eneo hilo kukiwemo mashambulizi ya ubaguzi dhidi ya raia na utumiaji wa silaha zilizopigwa marufuku. Mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mkubwa na kuchangia maelfu ya wakazi kukoseshwa makao.

Human Righs Watch pia imebaini kuwa wakati majengo mengi yaliharibiwa kutokana na  mashambulizi ya angani au mapigano, ni wazi kuwa majengo mengine mengi ambayo yalikuwa salama na watu wangeweza kuishi yalibomolewa bila sababu. Shirika hilo aidha linasema kuwakataza watu waliofurushwa kutoka nyumba zao dhidi ya kurejea bila kuwepo na sababu halali ya kiusalama au kuzipa makao jamii, zinafanya vikwazo hivyo kuwa visivyo na maana na kuchangia uhamisho wa lazima.

Picha: picture-alliance/AP Photo

Sheria ya kimataifa imetoa hakikisho la uhuru wa watu kutoka eneo moja hadi nyingine katika nchi ambayo wamo kisheria. Hatua ya serikali ya Syria kuwakataza watu kuingia na kutoka katika mji wa Qaboun na kuwazuia kurejea Darayya bila sababu maalum, ni ishara kuwa inakiuka majukumu yake ya kuhakikisha uhuru wa watu kuhama.

Shirika hilo la Huma RightsWatch limeitaka Urusi na mataifa mengine ambayo yanataka wakimbizi warejee, wanafaa kutumia uwekezaji wake na Syria kuhakikisha haki za mali ya watu waliokoseshwa makao wanaotaka kurejea zinalindwa, na serikali haibomoi mali yao kiholela na bila kuwapa chaguo mbadala.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/ https://www.hrw.org/news/2018/10/16/syria-residents-blocked-returning

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW