Watu 17 wajeruhiwa katika Ibada ya kumuaga Odinga
17 Oktoba 2025
Marais na wawakilishi wa nchi kadhaa za Kiafrika wameungana na maelfu ya waombolezaji katikaibada ya kitaifa, kuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga aliyefariki dunia wiki hii nchini India akiwa na umri wa miaka 80.
Wakenya wamejitokeza kwa wingi kumlilia Odinga tangu tangazo la kifo chake, na kuonyesha ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika medani ya kisiasa nchini Kenya. Maelfu ya watu waliujaza uwanja wa soka ambapo jeneza la Odinga lilikuwa limefunikwa kwa bendera ya taifa ya Kenya. Mke wake, Ida Odinga amewarai Wakenya kumuenzi mumewe kwa amani. ''Jambo moja ambalo najua Raila alilisimamia na akaendelea kulirudia, ni kwamba tunahitaji amani katika taifa letu, tunahitaji amani ndani ya nyumba zetu, na amani haitadumu katika hali ya machafuko. Kwa sababu hiyo nawaombeni leo, tumuomboleze Raila kwa amani," alisema Ida.
Duru zinasema kuwa watu 17 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kenyatta baada ya kukanyagana kwenye shughuli ya leo ya kumuaga Odinga. Wakenya watakuwa na fursa nyingine ya kuaga mwili wa Odinga mjini Kisumu kesho jumamosi, karibu na nyumba yake ya kijijini huko Bondo ambapo atazikwa Jumapili.