1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya waliokwama Cambodia waomba kurudishwa nyumbani

24 Februari 2026

Zaidi ya Wakenya 600 waliodai kushawishiwa kwenda Cambodia kwa ahadi za ajira, sasa wamefikisha suala hilo katika Mahakama Kuu ya Kenya wakiitaka serikali ya Kenya iwasaidie kurejea nyumbani.

Wahamiaji | Meli ya Geo Barents I
Wahamiaji wakisubiri kupokea msaada wa chakula katika meli ya Geo Barents baada ya kuokolewa kutoka Bahari ya Mediterania karibu na LibyaPicha: Ahmed Hatem/AP/picture alliance

Serikali ya Cambodia imewaagiza waondoke nchini humo kufikia Februari 28, 2026, la sivyo wakabiliwe na hatua za kisheria au hata kifungo gerezani. 

Nyaraka zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kenya jana Jumatatu, zinaeleza kwa undani mazingira ya kikatili ambayo Wakenya hao wanasemekana kupitia.

Wanaripotiwa kuzuiliwa katika jengo lililokuwa na ulinzi mkali, lenye uzio mrefu na waya wa seng'enge ili kuwazuia kutoroka.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo za mahakamani, walilazimishwa kufanya kazi bila kukoma kwa saa 16 na wengine walipata majeraha ya kuchomwa visu huku wengine wakiachwa bila matibabu.

Nyaraka hizo hata hivyo hazikubainisha moja kwa moja iwapo walikuwa wakifanya kazi katika vituo vya kulaghai watu mtandaoni, ingawa mamlaka za Cambodia imekuwa ikiendesha misako dhidi ya vituo hivyo katika wiki za hivi karibuni.

Kumeripotiwa ongezeko la vituo vya ulaghai wa mtandaoni katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia, ambavyo vinahusishwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

Hatari ya kuswekwa gerezani au kuendelea kunyanyaswa

Ripoti zinaeleza kuwa mamlaka za Cambodia zilivamia jengo walilokuwa wamefungiwa Wakenya hao, na watu waliokuwa wakiwazuia walifanikiwa kutoroka. Wakenya hao wamesema wanaishi katika makaazi ya muda, wanakosa chakula na huduma za matibabu.

Wakenya hao wameiomba mahakama kutoa amri ya dharura kuilazimisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya na taasisi nyingine za serikali kuwapa ulinzi wa kibalozi, wapate nyaraka za dharura za usafiri na serikali ya Kenya iwalipie gharama za kuwarejesha nchini.

Ombi lao linazingatia ulinzi wanaopewa kikatiba, wakiihimiza serikali itimize wajibu wake wa kulinda raia wake walioko nje ya nchi dhidi ya mateso, utumwa, na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kulingana na nyaraka za mahakama, mamlaka za Cambodia zimewataka Wakenya hao waondoke nchini humo ifikapo Februari 28, 2026, la sivyo wakabiliwe na hatua za kisheria au hata kifungo. Wakenya hao hata hivyo wameeleza kuwa hawawezi kumudu gharama za safari ya ndege kurejea Kenya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya amesema hana taarifa kuhusu kesi walioiwasilisha Wakenya hao mahakamani huku nayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Cambodia haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu kadhia ya Wakenya hao.

Mahakama Kuu ya Kenya inatarajiwa kusikiliza kesi hiyo leo, ambapo inaweza kutoa amri ya muda kuhusu iwapo serikali italazimishwa kuchukua hatua za haraka kuwaokoa raia wake.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW