1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya bado wanasuburi kumjua Rais mpya

11 Agosti 2022

Siku mbili baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, maafisa wa tume ya uchaguzi nchini humo bado wanakusanya matokeo ila bado hawajatangaza ni nani anayeongoza kinyang'anyiro cha urais katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kenia Wahlen Raila Odinga William Ruto
Mchuano ni kati ya William Ruto na Raila OdingaPicha: AFP

Vyombo vya habari nchini humo vinajaribu kufanya hesabu zao kivyao ila zinatokana na picha za fomu za matokeo tu kutoka zaidi ya vituo 46 elfu vya kupigia kura.

Jambo hilo limechangia kwa matokeo tofauti kuonyeshwa na vyombo tofauti vya habari suala lililochangia pakubwa kuwakanganya raia wa nchi hiyo katika kinyang'anyiro chenye ushindani mkali baina ya wagombea wawili wakuu, makamu wa rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Baadhi ya raia wana hofia kwamba matokeo tofauti yanayoonyeshwa na vyombo vya habari huenda yakachangia madai ya wizi wa kura ambayo yalisababisha machafuko katika chaguzi zilizopita nchini humo.

Mambo yazidi kunoga kwenye ushindani majimboni

Matokeo ya uchaguzi wa nyadhifa tafauti yanatarajiwa kutangazwa leo katika maeneo bunge ya Kisauni, Nyali na Mvita katika kaunti ya Mombasa. Hayo yakijiri, kwa mara ya kwanza katika historia, wapiga kura katika eneobunge la Lamu Mashariki, kaunti ya Lamu wamemchagua mbunge mwanamke katika uchaguzi mkuu uliokamilika Agosti 9.

Katika kaunti ya Mombasa, baadhi ya watu tayari wameanza kusherehekea ushindi wa baadhi ya wagombea kutoka jana hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa huku wengine wengi wakiendelea kusubiri matokeo ya kura kwa hamu na ghamu na baadhi wakiendelea na shughuli zao za kawaida.

Katika eneo bunge la Nyali na Kisauni, kuna uwezekano Mohammed Ali kutoka chama cha UDA akaregelea kiti chake cha ubunge wa Nyali huku mbunge wa zamani Rashid Bedzimba kutoka chama cha ODM akishinda kiti cha ubunge wa Kisauni ijapokuwa matokeo rasmi hayajatangazwa.

Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hamu kubwa iko kwa nani atakayemrithi Abdulswamad Nassir aliyekuwa mbunge wa Mvita kwa miaka 10 katika kiti hicho cha ubunge wa Mvita.

Lamu Mashariki washerehekea ushindi wa mwanamke wa kwanza kuwa mbunge 


Kando na haya, katika kaunti ya Lamu, wapiga kura katika eneobunge la Lamu Mashariki kwa mara ya kwanza katika historia wamemchagua mbunge mwanamke katika Uchaguzi mkuu uliokamilika Agosti 9.

Kisiwa cha Lamu nchini KenyaPicha: Sergi Reboredo/picture alliance

Ruweida Mohamed Obo wa Chama cha Jubilee alinyakua kiti hicho baada ya kuzoa kura 5,498 katika kinyang'anyiro kikali ambacho kilishirikisha wagombeaji wanne akiwemo mbunge anayemaliza muda wake Sharif Athman Ali wa United Democratic Alliance (UDA).


Akizungumza moja kwa moja na DW, Bi Obo, ambaye amehudumu kama mwakilishi wa wanawake wa Lamu kati ya 2017 na 2022, aliahidi kuwahudumia wapiga kura wake kwa bidii na kuhakikisha maendeleo yanapatikana Lamu Mashariki.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa wamefurahishwa na hatua hii na kusema kwamba ushindi wake ni dalili tosha kuwa wanawake wanaweza kuongoza. Walid Ahmed ni mkaazi wa Lamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW