1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya kuingia Afrika kusini bila viza

9 Novemba 2022

Kenya na Afrika Kusini zimefikia makubaliano ya kuwaruhusu raia wake kuingia ndani ya mipaka yao pasina kibali maalum kwa siku 90.

Kenia Nairobi Flughafen
Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Haya yanajiri wakati Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, anaizuru Kenya rasmi kwa mara ya kwanza kwa ziara ya siku mbili. Awali Kenya iliwaruhusu raia wa Afrika Kusini kuingia ndani ya mipaka yake pasina vibali ila hali ilikuwa tofauti kwa Wakenya.

Rais Ramaphosa alikaribishwa na mizinga 21 na kukagua gwaride la heshima kwenye Ikulu ya Nairobi kabla ya kuanza vikao na Rais William Ruto. Ziara hiyo ya siku mbili inalenga kuimarisha uhusiano, kuimarisha biashara, ushirikiano wa kisiasa na utamaduni.

Wakenya kuingia Afrika Kusini kwa siku 90 bila ya kibali chochote

Kiwanja cha ndege cha JohannesburgPicha: MICHELE SPATARI/AFP/Getty Images

Kuhusu suala la uhamiaji Rais Ramaphosa aliweka bayana kuwa Wakenya sasa wataweza kuingia nchini mwake pasina kibali kwa siku 90. Rais Ruto alibainisha kuwa wameridhia kuwarejesha wanaokiuka sheria na sera za uhamiaji ili kuilinda mipaka ya mataifa yao.

Viongozi wa mataifa hayo mawili wamepata pia fursa ya kutathmini hali ya uhusiano wa kidiplomasia. Ifahamike kuwa suala la Kenya kuhitaji visa kuingia Afrika Kusini ni tofauti na raia wa Afrika Kusini ambao hawahitaji kibali kuingia ndani ya mipaka ya Kenya.

Kenya na Afrika ya kusini wadau wakubwa wa safari za anga barani Afrika

Rais Cyril Ramaphosa aliwasili Jumanne jioni na kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya, Alfred Mutua na mwenzake wa Madini na Uchumi wa Rasilmali za Baharini, Salim Mvurya.

Soma zaidi:Mgomo wa marubani nchini Kenya waingia siku ya tatu

Ziara hii pia inajumuisha kikao cha masuala ya uchumi kitakachojikita kwenye biashara na uwekezaji kati ya Afrika Kusini na Kenya. Kenya na Afrika Kusini ndio mataifa pekee ya Afrika yaliyo na biashara kubwa ya usafiri wa ndege barani Afrika. Kadhalika, Kenya ni mshirika mkubwa wa biashara wa Afrika Kusini nje ya eneo la mataifa wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC.

DW Nairobi.