Wakenya waendelea kuomboleza kifo cha Raila Odinga
15 Oktoba 2025
Polisi wa India wamesema Odinga amefariki kutokana na mshtuko wa moyo. Mamia ya watu wamekusanyika kutoa heshima zao katika makazi ya Odinga jijini Nairobi, huku Rais William Ruto akitangaza siku saba za maombolezo na kuandaa mazishi ya kitaifa akimtaja Odinga kama mwanasiasa hodari wa Kenya:
" Ninatangaza kipindi cha siku saba za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti katika Jamhuri ya Kenya na katika balozi zetu zote nje ya nchi, ni ishara ya heshima kwake. Nimeahirisha shughuli zangu zote za umma kwa siku zijazo, na ninawaomba pia viongozi na watumishi wengine wote wa umma kufanya vivyo hivyo," alisema Rais Ruto.
Viongozi mbalimbali wa dunia kuanzia Afrika, Asia na kwengineko wametuma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi huyo ambaye ameiacha alama isiyofutika katika siasa za Kenya.