1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wahimizwa kulinda demokrasia yao

18 Novemba 2022

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye anawatolea wito Wakenya kuilinda demokrasia ili kuepuka kutumbukia kwenye lindi la maovu kama yanayotokea Uganda

Uganda Opposition Kizza Besigye Gerichtstermin in Kampala NO FLASH
Picha: AP

Kauli hizo zimejiri wakati wa kongamano la masuala ya haki za binadamu lililofanyika Nairobi. Ajenda ya kikao ni kuadhimisha miaka miwili tangu wahanga wa ukatili walipoteswa na maafisa wa usalama wa Uganda kabla ya uchaguzi mkuu. soma Kyagulanyi na Besigye kuungana na vyama vingine vitatu

Chini ya kauli mbiu ya tunasimama pamoja, wahanga wa ukatili wa Uganda walisimulia maovu yaliyowasibu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2020. Wahanga hao walielezea jinsi walivyoteswa, kupigwa, kukamatwa kwa nguvu na maafisa wa usalama ikiwa imesalia miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa Uganda. Kutilia mkazo simulizi hizo, kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alisistiza kuwa wako Kenya kupaza sauti zao na wala sio kuutishia utawala uliopo madarakani.

Dokta Besigye ambaye ni mzoefu wa siasa aliwarai Wakenya kulinda demokrasia kwa hali zote ili kuepuka kutumbukia kwenye hali inayowagubika waganda. Kuhusu kauli za hivi karibuni za majaribio ya kuondoa kipengele cha muda wa rais kuhudumu, Besigye aliweka bayana kuwa wanatiwa shaka na matamshi ya aina hiyo kwani ni ishara mbaya. Kauli hizo zilitolewa na mbunge wa Fafi Yakub Salah siku chache zilizopita.

soma Besigye amuonya Museveni asijaribu kubadili tena katiba

Utawala wa kidikteta

Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Akizungumza na kituo cha redio cha Spice FM siku ya Alhamisi, Dokta Besigye aliwatolea wito Wakenya kuwa macho kwani ndiyo mfano wa kuigwa wa demokrasia katika eneo la Afrika Mashariki. Kauli hizo zinaungwa mkono na Martha Karua, naibu kinara wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya anayeshikilia kuwa kamwe hatokaa kimya na kuruhusu udikteta kutawala.

Kongamano hilo la uwajibikaji wa masuala ya haki za binadamu linafanyika Nairobi kwani hali ya kisiasa nchini Uganda hairuhusu mikutano ya aina hiyo kufanyika. Wanaharakati na wanasiasa hao wa Uganda wako Kenya kwa mwaliko wa tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu, KNHRC. Mpinzani wa rais Museveni na mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliyehudhuria kongamano hilo lililofanyima kwenye majengo ya Ufungamano, alisisitiza kuwa wanachodai ni kutendewa haki na utu kudumishwa.

Itakumbukwa kuwa Bobi Wine anadaiwa kukamatwa na maafisa wa usalama siku ambayo maandamano yaliigubika Uganda mwezi wa Novemba mwaka 2020 ikiwa ni miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu. Wine alitarajiwa kuhutubia mhadhara eneo la Luula la Mashariki alipokamatwa. Duru zinaeleza kuwa watu wasiopungua 54 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye purukushani hizo.

 

//Thelma Mwadzaya

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW