1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya waomboleza vifo vya viongozi wawili

15 Februari 2021

Salamu za rambirambi zinaendelea kutolewa Kenya baada ya taifa hilo la Afrika Mashariki kupata misiba ya viongozi wawili mashuhuri wa kisiasa nchini humo Simeon Nyachae na Yusuf Hajji.

Afrika Kenia Beerdigung Simeon Nyachae, ehemaliger Politiker
Picha: Jared Omweri

Mazishi ya viongozi hao waliofariki kwa nyakati tofauti yanafanyika siku ya Jumatatu. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta pamoja na Naibu Rais William Samoei Ruto wanawaongoza Wakenya katika kumuaga kiongozi wa siasa za eneo la Gusii, Semion Nyachae aliyefariki tarehe 1 mwezi Februari mwaka huu akiwa na miaka 88 siku 5 tu kabla ya kufikisha miaka 89 akitazamiwa kuzikwa kijijini Nyosia kaunti ya Kisii.

Watu mbalimbali waliozungumza katika mazishi hayo wakiwemo wanafamilia wa Mzee Nyachae wamemkumbuka kiongozi huyo kama mtu shupavu katika masuala ya kitaifa na kifamilia huku ikikumbukwa kuwa Nyachae aliwahi kuwa waziri wa fedha kati ya miaka ya 1998 hadi 1999 kabla ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 na kuibuka wa tatu katika kinyang'anyiro hicho.

Rais Uhuru Kenyatta akiwa kwenye mazishi ya Simeon NyachaePicha: Jared Omweri

Hata hivyo, baada ya mazishi ya Nayachae, viongozi wa kisiasa wakiwemo Rais Kenyatta wanatazamiwa kuelekea hadi Nairobi  huko Lang'ata ambako watahudhuria mazishi ya Sseneta wa Garissa, Mohammed Yusuf Hajji, taarifa hizi ni kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani Dokta Fred Okeng'o Matiangi.

Hajji amefariki dunia siku ya Jumatatu baada ya kuugua kwa muda, siku chache tu aliporejea nchini kutoka Uturuki ambako alikuwa anapokea matibabu tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Kabla ya kifo chake Hajji alikuwa seneta wa jimbo la Garissa na vile vile mwenyekiti wa jopo kazi la kushugulikia Ripoti ya Maridhiano ya BBI na aliwahi kushikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi wa kitaifa katika serikali ya aliyekuwa rais wa tatu wa taifa la Kenya Mwai Emmilio Kibaki.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW