Wakenya wapigakura katika uchaguzi mpya wa rais
26 Oktoba 2017Wakenya wanapiga kura Alhamisi katika uchaguzi mpya wa rais ulioghubikwa na kususiwa kwa upinzani, ambako bila shaka kutampa ushindi Rais Uhuru Kenyatta, lakini akiwa na mamlaka iliyopungua kutokana na ushiriki mdogo na kasoro katika mchakato mzima, ambazo tayari majaji na tume ya uchaguzi wamekiri zina uwezakno wa kusababisha changamoto za kisheria.
Akiwahutubia wafuasi wake katikati mwa jiji la Nairobi, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alisema hatoshiriki katika uchaguzi huo mpya kwa sababu ya kushindwa kuwabadilisha makamishna wa tume ya uchaguzi baada ya mahakama ya juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali uliofanyika Agosti nane.
Muongo mmoja tangu watu 1,200 kuuawa katika uchaguzi mwingine uliobishaniwa, Wakenya wengi wamekuwa wakijiandaa na uwezekano wa kutokea vurugu nyingine. Odinga aliwasihi wafuasi wake kubakia nyumbani na kutokabiliana na polisi.
NASA kuwa vuguvugu la upingaji
"Tunafanya nini kesho? moja, tusishiriki kwa njia yoyote katika uchaguzi huu bandia. Pili, washawishi marafiki zako, majirani na kila mmoja asishiriki. Epukeni vituo vya kupigia kura na mbakie nyumbani," alisema Odinga mjini Nairobi siku ya Jumatano, na kuongeza kuwa "kuanzia leo tunaubadili muungano NASA na kuwa vuguvugu la upingaji."
Katika ngome za Odinga kama vile mji wa magharibi mwa Kenya wa Kisumu, hakukuwa na dalili za kuundwa kwa vituo vya kupigia kura, na maafisa wachache walioonekana walikuwa wamejikunyata katika ukumbi mtupu.
Afisa mmoja wa uchaguzi aliejitambulisha kwa jina moja la Evans mwenye umri wa miaka 26, aliifananisha hatua ya kutoka nje ya geti na sanduku la kupigia kura na kujitoa muhanga.
Kati ya maafisa 400 wa uchaguzi waliotarajiwa kuripoti kazini katika Shule ya sekondari ya Kisumu Lion's Club, ni 19 tu waliojitokeza. Maderava waliopaswa kuwapeleka na kuwarejesha kutoka vituoni pia walishindwa kutokea.
Muungano wa Odinga wa NASA, ambao umetuhumiwa kwa kuwanyanyasa maafia wa uchaguzi, unatarajiwa kutumia kigezo hicho kama ushahidi kwamba uchaguzi huu mpya, ulioandaliwa chini ya siku 60 ni batili na wa uongo.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati alisema wiki iliopita kuwa hawezi kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, akitolea sababu za uingiliaji wa wanasiasa na vitisho vya vurugu dhidi ya maafisa wa tume hiyo.
Kamishna moja wa tume alijiuzulu na kutoroka nchini akihofia usalama wake. Wakati wa mkutano wake alioufanya jana, Odinga alisema ataendeleza shinikizo la kufanyika uchaguzi mwingine chini ya tume mpya iliofanyiwa mageuzi ndani ya siku 90.
Mwito wa Kenyatta kwa Wakenya
Kwa upande mwingine, Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa taifa hilo, amebainisha wazi kuwa anauona uchaguzi wa leo kuwa halali. Akihutubia taifa hapo jana, Kenyatta aliwasihi Wakenya kujitokeza kwa ari kushiriki katika uchaguzi huo.
"Tukifanya hivyo tutazawadiwa kwa demokrasia imara na nafasi ya heshima ulimwenguni. Na tutamasika na utambuzi ambao sisi kama Wakenya tunastahili."
Uchaguzi huu unafuatiliwa kwa karibu katika kanda nzima ya Afrika Mashariki, ambayo inaitegemea Kenya kama kituo kikuu cha biashara na usafirishaji, na katika mataifa ya Magharibi, ambayo yanaiona Kenya kama mshirika muhimu katika vita dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia, na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.
Mhariri: Zainab Aziz