1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wapinga serikali kufuatilia watu kupitia simu

Saleh Mwanamilongo
27 Desemba 2023

Wanaharakati wa kutetea haki za mtandaoni wameonya hatua ya serikali ya Kenya kuanzisha mpango wa kuwafuatilia watu kupitia simu za mkononi ili kudhibiti bidhaa za bandia, utachochea serikali kuwachunguza watu wake.

Kenya | Mwanamume akizungumza na simu
Mwanamume akizungumza na simuPicha: Rodger Bosch/AFP/Getty Images

Wanaharakati hao walioshindwa katika kesi iliyochukua miaka sita, wakitaka serikali kuachana na mpango wake huo, wamesisitiza kwamba teknolojia hiyo itakiuka haki ya faragha ya watumiaji wa simu za mkononi.

David Indeje kutoka kwa taasisi ya teknolojia nchini Kenya ya KICTANet amesema mfumo huo ni mbinu ya serikali kuwachunguza watu wake.

Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali nchini Kenya Eliud Owalo alisema mwezi huu kwamba, serikali imepanga kuendelea na mpango wake wa kuzindua mfumo wa udhibiti vifaa DMS, ili kuziruhusu mamlaka kuipata nambari maalumu ya simu za mkononi na kuzuwia simu bandia.

Owalo aliendelea kusema kuwa hatua hiyo itapunguza kuenea kwa vifaa ghushi na kuibiwa kwa simu katika nchi hiyo, na kuzuia upotevu wa mamilioni ya dola kupitia ukwepaji kodi na simu za ulaghai, na kuimarisha usalama wa mtandao.

Soma pia:China na utamaduni wa kughushi na madawa bandia.

Kenya inatoza ushuru wa forodha na ushuru kwa simu zinazoagizwa kutoka nje pamoja na kodi ya mauzo ya rejareja. Pia inatoza matumizi ya mtandao na miamala ya kuhamisha fedha inayofanywa kupitia simu za mkononi, njia inayotumika sana kulipia bidhaa na huduma nchini.

Afisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CAK), ambayo inatekeleza mfumo wa DMS, ilisema shutuma kwamba teknolojia hiyo ili kiuka faragha ya raia zilikuwa habari potofu. Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema lengo la DMS ni kuwatenga na kuwanyima huduma

watu wanaoshikilia vifaa haramu. Hatua hiyo haimgusi mteja kibinafsi habari na data, aliendelea kusema. Mamlaka haijasema ni lini DMS itaanzishwa.

Kenya ni kitovu cha bidhaa bandia Afrika?

Tasnia ya mawasiliano ya simu GSMA kilisema kulikuwa na watumiaji milioni 489 wa simu ya mkono barani Afrika mnamo 2022 - karibu asilimia 43 ya idadi ya watu barani humo- na hii inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 692 ifikapo 2030.

Vijana wanatumia Internet kuleta matokeo chanya kwenye jamii

04:04

This browser does not support the video element.

Umuhimu wa simu mahiri hata hivyo unasalia kuwa kikwazo kikuu. Ingawa gharama ya simu mahiri imepungua sana, na utitiri wa vifaa kwa chini ya $100, wengi bado wanatafuta simu ya ubora wa juu kutoka kwa kampuni zinazojulikana, lakini bila gharama.

Kulingana na Shirika la Kupambana na Bidhaa Bandia nchini Kenya, Kenya ni kitovu kikuu cha bidhaa ghushi barani Afrika, na simu janja zikiwa zaidi ya nusu ya bidhaa zote feki nchini.

Soma pia:Kenya hupoteza mabilioni kila mwaka kutokana na bidhaa ghushi

Lakini vifaa hivi visivyo na leseni husababisha hasara kubwa ya kiuchumi uchumi kwa kukwepa kulipa kodi. Utafiti mmoja uligundua kuwa Kenya inapata hasara zaidi ya Shilingi bilioni 3 za Kenya sawa na dola milioni 20 kila mwaka ya ushuru ambao haujakusanywa kutokana na mauzo ya simu feki.

Simu ghushi, nyingi zikiwa zinatoka China, pia huleta hatari kubwa za kiusalama kwani mara nyingi hukosa ulinzi dhidi ya vitisho vya mtandao. Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali nchini Kenya Eliud Owalo aliiambia kamati ya bunge mwezi huu kwamba mfumo wa DMS utasaidia kupunguza hatari kama hizo.

Hata hivyo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema mamlaka itafute njia zingine za kuzuia kuenea kwa tatizo hilo la simu ghushi bila kukiuka haki ya faragha.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW