1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wasubiri kuupokea mwili wa Odinga

Shisia Wasilwa | Rashid Chilumba
16 Oktoba 2025

Kenya inaomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe wa upinzani Raila Odinga aliayeaga dunia siku ya Jumatano nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu.

Raila Odinga enzi za uhai wake
Raila Odinga enzi za uhai wake.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Mamia ya waombolezaji wamekusanyika kwenye makaazi ya mwanasiasa huyo mjini Nairobi kuifariji familia yake. Mwili wa Odinga utasafirishwa kwa ndege maalamu ya shirika la ndege la nchi hiyo kutoka India hadi Nairobi leo Alhamisi. 

Serikali iliwatuma maafisa wa ngazi ya juu kwenda India kwa ajili ya kuratibu kuurejesha nyumbani. Odinga aliyezaliwa mwaka 1945 alikuwa mtoto wa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya.

Miaka ya mwanzo ya harakati zake kisiasa ilishuhudia akifungwa jela au kukimbilia uhamishoni kutokana na utawala wa mkono wa chuma wa kiongozi wa wakati huo Daniel arap Moi. Atazikwa siku ya Jumapili katika kijiji alikozaliwa.

Hapo jana Jumatano, Rais William Ruto alitangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha Raila Amolo Odinga, aliyekuwa kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo.  Bendera za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kote nchini.

Katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja kutoka Ikulu jijini Nairobi, Rais William Ruto alitangaza kuwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Amolo Odinga, atazikwa kwa heshima kamili ya kitaifa. Rais aliongeza kuwa jina la Raila Amolo Odinga "litaandikwa milele katika simulizi ya jamhuri yetu, simulizi ya mapambano, kujitolea, ujasiri, utawala wa sheria, matumaini, na azma ya ubora.

Ruto alimwelezea Odinga kama mzalendo aliyejitolea maisha yake yote kutafuta haki nchini Kenya, mtu ambaye mawazo na misingi yake ilivuka mipaka ya siasa za kawaida.

"Tumempoteza mmoja wa viongozi wakuu zaidi barani Afrika — shujaa wa demokrasia, mpigania haki asiyeogopa na mwanaharakati thabiti wa utawala bora. Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za umma katika siku zijazo, ili niungane na taifa katika kipindi hiki cha maombolezo na tafakari ya kina,”.

Viongozi wa kimataifa wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi

Rais wa Kenya William Ruto Picha: Shisia Wasilwa/DW

Wakati huo huo, Rais Ruto ametangaza kwamba Serikali ya India imekubali kusaidia katika kuusafirisha mwili wa Raila Odinga kurejea Kenya kwa mazishi ya kitaifa.

Kamati ya maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu itakuwa ikiongozwa na Naibu Rais Kithure Kindiki pamoja na Seneta wa Siaya, Dkt. Oburu Oginga, kaka yake marehemu.

Ruto alifafanua zaidi kwamba ujumbe maalum wa maafisa wa serikali na jamaa wa familia, unaongozwa na Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, umeondoka mara moja kuelekea India kuratibu mipango ya usafirishaji wa mwili wa marehemu.

Wakati huo huo viongozi wa kimataifa wameenedelea kutuma salamu zao za rambirambi. Waziri mkuu wa India, Narendra Modi alikokuwa akitibiwa Raila, amesema amehuzunishwa sana na kifo cha rafiki yake mpendwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga. Alimwelezea Odinga kuwa "mwanasiasa wa hadhi ya juu” na rafiki mpendwa wa India ambaye alitambua na kuenzi urithi wa India na utamaduni wake.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, alitangaza kwamba kifo cha Odinga ni huzuni sio tu kwa Kenya bali kwa bara la Afrika, akimwelezea kama mtetezi wa amani na maendeleo. Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alimtaja Raila kuwa mwanasiasa mkongwe aliyeleta demokrasia, haki na huduma kwa umma na ataendelea kuishi.