Wakenya wasubiri matokeo kwa utulivu
8 Machi 2013Kwa mujibu wa taarifa zinazochapishwa moja kwa moja na mtandao wa gazeti la Daily Nation la Kenya, kufikia sasa tayari majimbo 226 kati ya 290 yameshahisabiwa, huku Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta akiongoza kwa asilimia 50.1 mbele ya mpinzani wake wa karibu Waziri Mkuu Raila Odinga mwenye asilimia 43.4.
Hata hivyo, matokeo hayo yanatoka kwa kasi ndogo mno na hivyo kusababisha IEBC kutupiwa lawama kwamba ina njama ya kuiba kura, tuhuma ambazo mwenyekiti wa tume hiyo, Ahmed Issack Hassan, anazikanusha, akisema kwamba tume yake haijashinikizwa na mtu yeyote kuchelewesha au kutoa uamuzi kupendelea upande mmoja.
“Ningetaka kuwahakikishia kwamba kwa niaba ya tume, mwenyekiti na wajumbe wengine wa tume hii, makamishna na wafanyikazi wa tume hawaegemei upande wowote. Tumekula kiapo kuhakikisha tunadumisha sheria kwa kutoa huduma bila upendeleo”. Alisema Hassan.
Waangalizi waiunga mkono IEBC
Na licha ya wananchi kulalamika kwamba muda waliosubiri matokeo hayo mrefu mno, waaangalizi wa uchaguzi huo wameipongeza IEBC kwa kazi nzuri inayoifanya.
Dk. David Matsanga, mtaalam wa usuluhishaji mizozo kutoka nchi jirani ya Uganda, amesema mwenyekiti wa IEBC hastahiki kushinikizwa kutoa matokeo hayo.
Kenyatta na mgombea mwenza wake, William Rutto, wanakabiliwa na mashitaka ya jinai katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague wakihusishwa na ghasia zilizozuka punde tu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Habari kutoka ICC zinasema kwamba mahakama hiyo imeahirisha tarehe ya kuanza kwa kesi ya Kenyatta na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Francis Muthaura, kutoka tarehe 11 Aprili hadi tarehe 9 Julai mwaka huu.
Jopo la majaji watano wanaosikiliza kesi hiyo walikubali ombi la wakili Francis Kirimi wa Muthaura na Kenyatta kuahirisha kesi hiyo.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef