Wakenya waulaki mwili wa Odinga
16 Oktoba 2025
Kwa mujibu wa familia yake Raila aliacha wosia, akisema kuwa azikwe ndani ya kipindi cha siku tatu.
Serikali imetangaza kusimamisha shughuli zote siku ya Ijumaa, ili Wakenya wapate nafasi ya kutoa heshima zao kwa mwamba huyo ambaye wengi wanasema ni baba wa demokrasia nchini.
Mamia ya Wakenya katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta waliimba nyimbo za kumsifu Raila, wakiwa na matawi na mabango yenye picha ya marehemu.
Mwili kutazamwa uwanja wa Kasarani
Rais William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na wanafamilia ni miongoni mwa watu walioupokea mwili wa Odinga mapema Alhamisi ambao ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Lee.
Hata hivyo mipango ya kuupeleka mwili huo katika Bunge la taifa ilibadilishwa na badala yake kupelekwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani kutokana na vurugu zilizoshuhudiwa.
Wakenya wa matabaka mbali mbali watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho. Naibu Rais Kithure Kindiki, alisema kuwa Marehemu Raila Odinga alitaka azikwe baada ya siku tatu pindi angefariki.
"Maziko ya hayati mheshimiwa Raila Odinga yatafanyika jumapili hii, yataendeshwa na kanisa la Kiangalikana ambalo alikuwa muumini,” alisema Kindiki.
Mwili huo utarejeshwa katika hifadhi ya Lee mwendo was aa kumi na moja jioni. Baada ya hafla hiyo, mwili utaelekezwa nyumbani kwake Karen kwa mapumziko ya usiku mmoja.
Raila kuzikwa makaburi ya familia
Siku ya Jumamosi mwili utaondolewa Nairobi kuelekea Kisumu, ambapo wananchi watapata nafasi ya kuuaga katika Uwanja wa Moi.
Baadaye, mwili utasafirishwa kwa barabara hadi Bondo kwa mapumziko ya usiku. Siku ya Jumapili Mazishi yatafanyika kwa kufuata taratibu za Kanisa la Anglikana la Kenya nyumbani kwake Bondo.
Kwa mujibu wa mpango wa mazishi, Raila atazikwa katika makaburi ya familia Kango Ka Jaramogi, Bondo, karibu na makaburi ya baba yake Jaramogi Oginga Odinga na mwanawe Fidel.
Wakati huo huo Baraza Kuu la Chama alichoongoza Raila cha ODM kimemchagua kakake Oburu Odinga kuwa kaimu kiongozi wa chama hicho kwa wakati huu.