Wakenya wenye asili ya Kisomalia waishi kwa hofu baada ya mashambulizi
28 Novemba 2013Raia hao wengi wao wanaoishi katika eneo la Garisa mpakani mwa Kenya na Somalia, wanalalamikia mlolongo mrefu wa kupata vitambulisho vya uraia, huku wakiendelea kukamatwa na kuteswa kwa kukosa vitambulisho halali.
Kama ilivyo kawaida, kumaliza elimu ya sekondari ni wakati ambao hufurahiwa na kila mmoja, lakini kwa Khadija Jabril, mwenye asili ya Kisomalia, anayeishia katika eneo hilo, lililopo Kaskazini mwa Kenya, sherehe za kumaliza shule zimejawa na hofu.
Atakapomaliza mitihani wake mwezi ujao, kitambulisho chake cha shule kitakwisha muda wake,lakini hana kitambulisho cha taifa, mbali ya kwamba amepeleka maombi ya kupata kitambulisho hicho mara nne bila mafanikio.
Bila kuwa na vitambulisho maalum vya kumtambulisha hawezi kuomba kazi, wala kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, na hatari zaidi atakuwa hatarini kupelekwa mahakamani kwa makosa ya uhamiaji haramu, au kutuhumiwa kuhusishwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Shambulizi la Al Shabaab liliua watu zaidi ya watu 60
Kundi la kigaidi la Al shabaab la nchini Somalia linadaiwa kuimarisha mitandao nchini Kenya na kufanya shambulizi katika jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi ambapo zaidi ya watu 60 waliuawa.
Khadija anasema, hali ya sasa ikiwa mtu hana kitambulisho anatiliwa shaka ikiwa ni raia wa Kenya au la, kwa hivyo inambidi akae ndani na kutoka nyakati za usiku.
Vijana wengi wa Somalia, Kaskazini mwa Kenya wanakabiliwa na changamoto katika kupata vitambulisho, kutokana na mlolongo uliopo kuomba uraia, katika nchi hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali ya kuwasilisha makaratasi yote yanayohitajika, kuna hatua nyingine nne muhimu za kufuata , na mwisho kupata utambulisho kutoka kwa kiongozi wa kitongoji, atakayethibitisha ikiwa aliyepeleka maombi ni raia wa Kenya, kutokana na taratibu zilizowekwa kupata uraia wa Kenya.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya nchi zilizopo katika pembe ya Afrika, Abdullahi Boru, raia hao pia wanakabiliwa na kubaguliwa kiuchumi, pia hawana miundo mbinu bora, huduma duni za matibabu, sambamba na kiwango kikubwa cha ukosefu wa jira.
Kwa mujibu wa Sheikh, Hassan Massad wa Garisa, watu katika eneo hilo kwa sasa wapo kati kati ya vizuizi dhidi ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab na vikosi vya usalama vya Kenya.
Sheikh Hassan anasema kuwa kwa sasa wanaishi katika hali ya wasi wasi na kilichobaki ni kumwomba Mungu.
Kuna jumla ya watu milioni 2.3
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2009, kuna jumla ya watu milioni 2.3 wenye mchanganyiko wa makabila mbali mbali ya Kisomali na ya Kenya, ikiwa ni sawa na asilimia 6 ya wakaazi wa eneo hilo, wengi wao wakiwa ni wafugaji, ingawa wengi wanaegemea uraia wa Kenya.
Huku hatua ya kupata vitambulisho ikiwa ni ndefu na kufanya raia wa Kisomalia kuishi kwa hofu, zoezi la kukamatwa kwa watu wasiokuwa na vitambulisho linaendelea katika maeneo mbali mbali, na wengine wakidai kuachiwa kwa kutoa rushwa na wengine kukamatwa.
Hilo linathibitishwa na Abdirahan Barale ambaye anasema kuwa kuna wakati alikamatwa na kuwekwa ndani alipokwenda kumjulia hali bibi yake aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Kenyatta, ambapo aliwekwa ndani kwa siku mbili, huku akiambulia kipigo cha polisi kabla ya kuachiwa huru.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Binadamu la Human Rigtht Watch, lenye makao yake mjini New York, Leslie Lefkow, mara nyingi kunapokuwa na hali ya wasi wasi wa usalama katika eneo hilo la Kaskazini mwa Kenya, kunakuwepo na hali ya kulipiza kisasi dhidi ya walinzi wa usalama kwa kuwapiga ovyo watu na wakati mwingine wakiwatesa, hasa wale wenye asili ya Kisomali.
Mwandishi: Flora Nzema/DPAE
Mhariri: Mohamed Khelef