1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakfu wa Thabo Mbeki wakosoa uchaguzi wa Tanzania

24 Novemba 2025

Wakfu wa Thabo Mbeki, rais wa zamani wa Afrika Kusini umetoa tamko kuhusu uchaguzi wa hivi karibuni Tanzania na kueleza kwamba ulikosa misingi na miongozo inayosimamia chaguzi za kidemokrasia katika Jumuiya ya SADC

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo MbekiPicha: MICHELE SPATARI/AFP

Tamko hilo la Wakfu wa Thabo Mbeki limetolewa jana ikiwa ni wiki kadhaa tangu kushuhudiwe ghasia za wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania.  Limerejelea matamko yaliyotolewa na misheni za waangalizi wa uchaguzi EOM, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC na Umoja wa Afrika kuhusu yale yaliyojiri katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Kulingana na tamko hilo, Jumuiya hizo zilihitimisha kwamba uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 Tanzania ulishindwa kutimiza kanuni na miongozo inayosimamia chaguzi za kidemokrasia za SADC na AU pamoja na viwango vya kimataifa. Limenukuu matamko ya SADC na EOM, kwamba wapiga kura nchini Tanzania walishindwa kutumia uhuru wao wa kidemokrasia. Taarifa hiyo imeongeza kwamba kwa mujibu wa waangalizi wa SADC na AU matokeo ya rais na bunge yaliyotangazwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi INEC sio kielelezo cha kweli cha Watanzania.

Maandamano ya uchaguziPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Max Boqwana ni afisa mkuu mtendaji wa Wakfu wa Thabo Mbeki. "Tanzania daima imekuwa mfano wa kuigwa katika suala la kuunda upya na kuendeleza bara letu. Kwa hiyo wakati mambo yaliyotokea Tanzania wakati wa uchaguzi hasa kuwekwa mahabusu kwa viongozi wa vyama vya upinzani, vurugu ambazo zimesababisha vifo vya watu kadhaa lakini pia watu wengi ambao wamejeruhiwa. Ni dhahiri kabisa kumesababisha wasiwasi mkubwa sana kwetu," alisema Boqwana.

Tamko hilo limedokeza kwamba yote hayo yamechangia hitimisho la kutia wasiwasi kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasasa haina serikali halali, likidokeza kuwa utawala wa sasa umesimikwa kwa watu kupitia mchanganyiko wa nguvu na njia za ulaghai. Hali hiyo imezidishwa na ripoti zinazoendelea na zenye kusitisha za vurugu za kimfumo dhidi ya wapinzani wa CCM, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara na mauaji, limesema tamko hilo.

CCM yatoa kauli nzito kuhusu vurugu zilizotokea Tanzania

02:02

This browser does not support the video element.

Hata hivyo rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya uchaguzi huo alisema kwamba alipokea mapendekezo yaliyotolewa na waangalizi wa jumuiya hizo lakini hawatokubali maagizo. "Nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifu tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu mkubwa, tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo ya kutuelekeza nini cha kufanya tumeyakataa," alisema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wakfu huo pia umeungana na baadhi ya watu nchini Tanzania wanaopendekeza maridhiano na kupendekeza mazungumzo ya kitaifa, yenye kuaminika, jumuishi na huru kama njia sahihi ya kuliponya taifa sambamba na kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa.

Wakfu wa Thabo Mbeki pia umetaka taifa lijibu maswali magumu ikiwemo nini kilichokwenda kombo, nini kifanyike ili kuirudisha nchi katika njia sahihi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW