1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi 15,000 wa Kipalestina wakwama Iraq

Mohamed Dahman26 Aprili 2007

Maafisa wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani wamethibitisha wiki hii kwamba wamekuwa katika majadiliano na Israel na serikali ya jimbo la Wakurdi nchini Iraq juu ya uwezekano wa suluhisho la kuwatafutia makaazi mapya wakimbizi wa Kipalestina wanaokadiriwa kufikia 15,000 ambao hivi sasa wamekwama nchini Iraq.

Alama ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ambalo linawatambuwa wakimbizi wa Kipalestina waliokwama Iraq......kishindo ni mahala pa kuwapeleka.
Alama ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ambalo linawatambuwa wakimbizi wa Kipalestina waliokwama Iraq......kishindo ni mahala pa kuwapeleka.Picha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari msaidizi wa waziri wa mambo ya nje ya Marekani katika Ofisi inayoshughulikia masuala ya Idadi ya Watu ,Wakimbizi na Uhamiaji Ellen Sauerbrey amesema kwa wakati huu hawakuweza kupata itikio zuri lakini wanaendelea kulishughulikia suala hilo na kua hakuna mjadala kwamba kundi la wakimbizi hao ni rahisi sana kuathirika na kwamba hawana mahala pa kwenda.

Usalama wa wakimbizi wa Kipalestina nchini Iraq umedhoofika sana tokea uvamizi uliongozwa na Marekani nchini humo hapo mwaka 2003.Maafisa wa Palestina na wa haki za binaadamu wanasema wakimbizi hao ambao takriban wote ni wa madhehebu ya Wasunni wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili, wakinyanyaswa na kuhamishwa kwenye nyumba zao na makundi ya wanamgambo wa Kishia yanayotanga tanga na polisi ya Iraq katika jitihada za kuwafukuza kutoka Iraq.Kwa mujibu wa repoti ya Shirika la Haki za Binaadamu la Human Right Watch wizara ya ulinzi ya Iraq imehusishwa katika kuwakamata ovyo, kuwatesa, kuwauwa na kutoweka kwa Wapalestina hao.

Jay Zimmerman ofisa mipango wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani kwa Iraq amesema wamekuwa wakilizungumzia suala hilo na Mamlaka ya Palestina na wanatambuwa kwamba hususan Wapalestina walioko Baghdad wako kwenye hali inayowafanya kuwa rahisi kuathirika.

Zimmerman hakusema wizara yake imekuwa na mawasiliano na maafisa gani wa Mamlaka ya Palestina kwa vile serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina inajumuisha kundi la Hamas linalohesabiwa na Marekani na Israel kuwa ni kundi la kigaidi.

Kabla ya uvamizi wa Marekani wa mwaka 2003 Wapalestina wanaokadiriwa kufikia 35,000 walikuwa wakiishi nchini Iraq wakiwa ni watoto na wajukuu wa Wapalestina waliokifuata kikosi cha Iraq ambacho kilipigana katika vita vya kwanza kati ya Waarabu na Israel hapo mwaka 1948.Juu ya kwamba walikuwa wamenyimwa haki ya kupatiwa uraia wa Iraq Wapalestina hao walikuwa wakipendelewa na Saddam Hussein ambaye alikuwa akiwatumia kama zana ya propaganda kuimarisha hisia ya utaifa ya Uwarabu dhidi ya Israel.

Hivi sasa takriban Wapalestina 1,200 bado wamekwama katika kambi tatu za mpakani karibu na mpaka wa Syria na Iraq wakati waliobakia kati ya 15,000 hadi 34,000 wamekwama mjini Baghdad.

Nchi jirani za Syria na Jordan ambazo zimepokea idadi kubwa ya wakimbizi milioni mbili wa Iraq ikiwa ni matokeo ya mzozo wa Iraq zimefunga mipaka yao kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Ingawa Wapalestina walioko nchini Iraq hawako chini ya mamlaka ya UNRWA ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa lenye kutowa misaada ya kibinaadamu kwa wakimbizi wa Kipalestina na familia zao wanatambuliwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa.

Kwa vile Marekani imesaini makubaliano ya mwaka 1951 juu ya hadhi ya wakimbizi ina dhima muhimu ya kutimiza.

Bill Frelick mkurugenzi wa sera ya wakimbizi wa Shirika la Haki za Binaadamu la Human Right Watch anasena tayari wanatambuliwa kuwa ni wakimbizi na wakati Marekani inaikalia Iraq kwa mabavu ina uwezo ya kuwahamisha kuwaingiza kwenye ndege na kuwaondowa nchini Iraq lakini suala je ndege hiyo itakwenda kutua wapi ?

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW