Wakimbizi Afrika kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula-UN
19 Juni 2022Taarifa ya Shirika la Chakula Ulimwenguni, WFP iliyochapishwa Jumapili mjini Roma, Italia, imesema kuwa robo tatu (75%) ya wakimbizi wanaohudumiwa na Umoja wa Mataifa katika ukanda wa mashariki mwa Afrika, wamepunguziwa mgao wa chakula kwa hadi asilimia 50. Kwa mujibu wa shirika hilo, walioathirika zaidi ni wale wanaotafuta hifadhi katika kambi za nchini Ethiopia, Kenya, Sudan Kusini na Uganda.
Soma zaidi: UN: Vita vya Ukraine kusababisha mgogoro wa chakula duniani
''Tumelazimika kuchukua hatua za kuvunja moyo za kupunguza kiwango cha chakula tunacowapatia wakimbizi, ambao msaada wetu ndilo tegemeo lao pekee la kuishi,'' amesema Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley.
Mkurugenzi huyo mkuu ameongeza kuwa raslimali zilizopo hazikidhi mahitaji ya msaada wa chakula yanayoongezeka kwa kasi kote duniani.
Afrika Magharibi nako hali si shwari
Upande wa Afrika Magharibi, hususan nchini Burkina Faso, Kameruni, Chad, Mali, Mauritania na Niger, WFP nako imepunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi.
Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa limeonya juu ya kuvurugika haraka kwa utaratibu wao wa msaada katika mataifa mengine ya Afrika, yakiwemo Angola, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kongo, Tanzania na Zimbabwe.
Soma zaidi: Asilimia 40 ya watu wa Tigray wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula
Jumanne iliyopita, WFP ilitoa rai ya kupatiwa dola milioni 426 ili iweze kuepusha janga la njaa nchini Sudan Kusini, ambako miaka mingi ya ghasia na mafuriko imewafanya watu wengi kuyapa kisogo makaazi yao.
Ilisema katika taifa hilo changa linaloandamwa na mizozo, theluthi mbili (takribani 66%) ya wakaazi wote wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku wapata milioni 8.3, wakimbizi miongoni mwao, wakitarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu.
Vita vya Ukraine vyaifanya hali kuwa mbaya zaidi
Mzozo wa vita nchini Ukraine umezidisha makali ya tatizo la wakimbizi duniani pamoja na kitisho cha njaa. Sio tu kwamba vita hivyo vimesababisha wakimbizi wapya zaidi ya milioni sita walioyahama maeneo ya mapigano, bali pia vimechochea ongezeko kubwa la bei ya bidhaa muhimu kama nafaka.
Soma zaidi: WFP yaomba dola milioni 121 kuwasaidia watu wa Cabo Delgado
Jana Jumamosi, Mkuu wa diplomasia katika Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliiuhumu Urusi kufanya chaguo la kutumia mauzo ya nafaka kama silaha ya vita, kwa kuzuia usafirishaji wa ngano na mazao mengine kutoka Ukraine kwenda katika nchi maskini.
Kabla ya uvamizi wa Urusi, Ukraine ilikuwa mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa kuuza nje mazao ya chakula, ikichangia asilimia 12 ya mauzo ya ngano, asilimia 15 ya biashara ya mahindi, na karibu asilimia 50 ya mafuta ya alizeti yanayouzwa kwenye soko la dunia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema vita hivi vya Ukraine vinaweza kuwasukuma makumi ya mamilioni ya watu kwenye ukingo wa njaa.
-AFP