1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi Kakuma, Dadaab waitaka Kenya kulegeza vikwazo

Michael Kwena19 Juni 2023

Wakimbizi wanaoishi katika kambi za Kakuma na Daadab nchini Kenya, wanazitaka mamlaka nchini humo, kulegeza vikwazo vilivyowekwa dhidi ya wakimbizi ili waendeshe biashara zao.

DW Akademie | Straße in Kakuma in Kenia
Picha: Laura Wagenknecht/DW

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya wakimbizi,idadi kubwa ya wakimbizi kutoka kambi ya Kakuma,wanaitaka serikali ya kenya kuwapa vibali vya kuendesha biashara ili nao pia wachangie katika mapato ya taifa.

Idadi kubwa ya vijana wakimbizi ,wanajihusisha na biashara ya bodaboda hapa Kakuma japo wanatamani serikali iwape stakabadhi zitakazowawezesha kuondoka kambini na kujihusisha na biashara zingine.

Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab kaskazini mwa KenyaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kulingana na Ramadhan Lumumba Ramadhan mkimbizi anayeishi katika kambi hii ya Kakuma,wakati umewadia kwa serikali kuwaruhusu wakimbizi wawe na uhuru wa kuendesha biashara zao sehemu yoyote nchini.

"Iwapo serikali inaweza kutenga sehemu nje ya kambi ya Kakuma kwa ajili ya wakimbiz kuendeshea biashara basi itakuwa bora zaidi…”

Kambi ya Kakuma ina zaidi ya wakimbizi laki mbili na wengi wa wakimbizi hao wanalazimika kutegemea misaada kutoka mashirika ya kijamii kwa kuwa hawana biashara za kuwaingizia mapato huku shirika la umoja wa mataifa la kuwashugulikia wakimbizi UNHCR likiwa mfadhili mkuu.

Idadi kubwa ya wakimbizi wameshindwa kutafuta ajira katika taasisi mbalimbali humu nchini kwa kukosa kuwa na vibali vinavyowatambua kirasmi hapa nchini kama anavyoelezea mkimbizi huyo aliyeomba jina lake libanwe.

"Sisi kama wakimbizi tupewe zitambulisho ili tuwe kama wakenya. Wengine wetu hawawezi kurudi katika mataifa walikotoka lakini wakipata vitambulisho, itakuwa ni afueni kwao...”

Mkakati wa kuwajengea wakimbizi nyumba za kudumu Kenya

02:00

This browser does not support the video element.

Serikali ya Kenya kwa upande wake imekiri kuwa na ufahamu kuhusu changamoto wanazozipitia wakimbizi katika kambi za Kakuma na Dadaab ila mipango inaendelea ya kuwashugulikia ipasavyo.

Kulingana na kamishna anayesimamia masuala ya wakimbizi nchini John Burugu,serikali inaendelea kuchukua takwimu za wakimbizi na kwamba,hivi karibuni watapewa nyaraka zinazohitajika ili kuwa na uwezo wa kujiendeleza wenyewe.

"Tunaelekea katika kizazi cha tatu cha wakimbizi na hawawezi kuendelea kusalia vivyo hivyo,na kwa hivyo,kupewa kitambulisho ni muhimu lakini hilo litawezekana tu baada ya sisi kusafisha deta ya wakimbizi wote. Lazima tuwe na mpango kwa sababu suala la kiusalama pia ni sharti lizingatiwe”

Serikali kwa wakati huu inaendelea na mpango wa kuwajengea wakimbizi makaazi katika eneo la kaloyobeyei kama sehemu ya kuwaunganisha wakimbizi na Jamii zinazowahifadhi.

Siku ya wakimbizi duniani huadhimishwa kila tarehe ishirini juni kuwasheherekea wakimbizi katika mataifa yote ulimwenguni kauli ya mwa huu ikiwa ni kuwa na matumaini mbali na nyumbani yaani hope away from home.

Michael Kwena, DW Kakuma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW