1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi kisiwani Malta: Wamefika lengo lao?

Ute Schaeffer / Maja Dreyer19 Novemba 2007

Kati ya nchi za Ulaya zinazopakana na bahari ya Mediterania, kisiwa kidogo cha Malta chini mwa Italia inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya kutokana na idadi kubwa ya wahamiaja wanaotoka bara na Afrika.

Bandari ya Malta
Bandari ya MaltaPicha: Illuscope

Jonas, kijana wa umri wa miaka 28, hakuwa na sababu hata moja kukaa katika nchi yake ya Eritrea. Licha ya kuwa na elimu ya juu na kufanya kazi katika kampuni ya mafuta hakuweza kuilisha familia yake. Miaka mitatu iliyopita alikimbilia Malta. Jonas anasema: “Kuna shinikizo kubwa kwa vijana kujiunga na jeshi ambapo lakini watabakia maisha yote. Vinginevyo maisha ni magumu. Huwezi kusema wazi maoni yako juu ya serikali, ama utapelekwa gerezani. Tuna udikteta Eritrea. Ndiyo sababu niliamua kwenda Ulaya.”


Lakini kijana Jonas hakuweza kufikiria kabla yale ambayo yangetokea kwenye safari. Wengi walioenda naye katika boti walianguka baharini au walikufa kutoka na kupoteza nguvu zao. Meli nyingi za kusafirisha wakimbizi zilizama njiani kwenda Italia.


Baada ya kufika Malta, Jonas wa kutoka Eritrea alikaa katika kambi ya wakimbizi wa muda wa mwaka mzima. Leo anaishi katika kambi ya kanisa katoliki. Huko anapata yale anayohitaji kuishi, ana uhuru wa kukaa nchini Malta kwa muda lakini ni vigumu kupata kazi. Lengo lake hajalifikia, anasema Jonas: “Lengo langu lilikuwa kwenda Ulaya kupata elimu na kazi nzuri. Watu wa Eritrea ni watu wasio na matumaini. Mimi nilitafuta njia mpya na kusaidia kabila langu. Nchi hii lakini ni ndogo sana na kuna wakimbizi wengi. Hakuna njia ya kwenda mbali wala kupata elimu. Hata ukiwa na ujuzi fulani huwezi kuutumia. Kazi zilizopo ni kazi ngumu tu kwa watu bila ya elimu.”


Leo lakini, Jonas anajiuliza kama wale walioshikwa na polisi wa baharini na kurudishwa nyumbani, pengine wana maisha bora kuliko hao waliofika Malta bila ya kufika kweli.


Kisiwa kidogo cha Malta kinakaribia kujaa wakimbizi. Hata hivyo, bado kinatekeleza sera huru ya kuwapokea na kuwasaidia wakimbizi. Zaidi ya nusu ya wahamiaji wanaofika huku kwa njia zisizo halali wanaruhusiwa kukaa kwa muda fulani, hususan wale wanaotoka eneo la vita, mfano Somalia. Wale wanaokubaliwa kukaa kwa muda, kawaida wanaishi katika nyumba za kanisa kama ile anapoishi Jonas.


Ukizungumza na wakimbizi wengine utafahamu matokeo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika. Wakimbizi kutoka Ivory Coast, Somalia, Ethiopia na Eritrea waliunda kundi la kusaidiana, wanajifunza Kiingereza kwa pamoja na kupeleka watoto wao shuleni.


Kijana Jonasa aliyeongoza mazungumzo na mke wa rais Köhler, Bi Eva-Luise Köhler anaziomba nchi za Ulaya ziwajali zaidi wakimbizi na kuwasaidia.


Serikali ya Malta inataka wakimbizi wanaofika kwenye pwani za nchi za Mediteranian wapelekwe katika nchi zote za Umoja wa Ulaya kulingana na ukubwa wa nchi hizo. Pia, inataka nchi nyingine zichangie katika kulinda pwani na bahari. Katika ziara yake nchini Malta, rais Köhler wa Ujerumani alisema juhudi za kupambana na changamoto hiyo zitachukua muda mrefu. Uhamiaji utapungua tu ikiwa hali katika nchi za Kiafria itaboreka. Inabidi watu waweze kuishi katika nchi zao. Kwa hivyo, muhimu zaidi ni maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW