Wakimbizi wa Goma wana hali mbaya
30 Mei 2013Ukitembelea makambi ya wakimbizi, iwe yale yaliyotayarishwa na serikali kwa ajili ya kuwahifadhi raia wanaokimbia vita au majengo ya shule yanayowahifadhi wakimbizi bila ya kutengwa na serikali, utapigwa na bumbuwazi kwa jinsi wakimbizi wanavyoishi kama wanyama.
Katika baadhi za kambi za wakimbizi hakuna mahema, blanketi wala vifaa vya matumizi ya nyumbani. Baadhi ya watoto wameshadhohofika kutokana na kukosa chakula.
Wamoja wao wanalala kwenye mawe ya volkano, na mama zao wakiwa hawana chochote kwa ajili ya mlo kwa watoto wao zaidi ya kulia pamoja na watoto wao wanaoumwa na njaa.
Wakimbizi kwenye kambi ya Kituku katika mji wa Goma wamefikia umbali wa kuomba kurudi makwao , ili wakafie huko katika vita, badala ya kufa kwa njaa na maradhi kutokana na majanga kambini.
Tayari Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na maswala ya kiutu na misaada ya dharura, Bibi Kyung Wang Kang, ametembelea kambi ya wakimbizi ya Sotraki, ambako wakimbizi si chini ya elfu tatu wanajihifadhi. Lakini tangu kufanyika kwa ziara hiyo, hakuna hata shirika moja lililojitokeza kuwasaidia wakimbizi hao.
Vita vya kila mara katika mkoa wa Kivu ya kKaskazini vimesababisha maelfu ya watu kuyahama makaazi yao na kukimbilia kambini, lakini hadi sasa wengi wao hawajui ni siku gani watapata chakula.
Mwandishi: John Kanyunyu /DW Goma
Mhariri: Mohammed Abdulrahman