1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa kisomali na mama wa watoto 38 magazetini

Oumilkheir Hamidou
12 Mei 2017

Hofu za kurejeshwa nyumbani wakimbizi wa Somalia, jinsi viongozi wengi wa Afrika wanavyofurahikia mwongezeko mkubwa wa wakaazi katika nchi zao na hadidhi ya Mama Afrika, raia wa Uganda aliyezaa watoto 38 Magazetini

Spanien Melilla Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Palacios

 

Tunaanza na gazeti la die Tageszeitung linalomulika ule mpango wa kuwarejesha makwao wakimbizi nchini Ujerumani. "Kwa khiari ndo ina maanisha nini"? Hicho ni kichwa cha maneno cha ripoti ya mhariri wa gazeti hilo Marina Mai anaesimulia jinsi wasomali wanaoomba kinga ya ukimbizi walivyoingiwa na hofu wasije wakarejeshwa makwao. Eti baada ya wakimbizi wa Afghanistan na wasomali pia wanaoomba kinga ya ukimbizi watarejeshwa makwao? Hadi wakati huu maafisa wa serikali ya Ujerumani hawakumlazimisha  msomali yeyote anaetokea katika nchi hiyo iliyoteketezwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, mashambulio ya kigaidi na njaa kurejea katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Lakini shinikizo linazidi kukuwa; mara kwa mara wakimbizi wa Somalia wanatakiwa warejee nyumbani kwa khiari la sivyo watalazimika kurejeshwa nyumbani au katika nchi nyengine itakayokubali kuwapokea.

 Al Shabab hawana haja ya kuwaandama wakimbizi wasiokuwa na umuhimu wowote

Gazeti la die Tageszeeitung linazungumzia kisa cha kijana wa miaka 18 Ahmed Muse anaeishi mjini Berlin ambae gazeti linasema alitekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabab alipokuwa mdogo na kulazimishwa kujiunga na mafunzo ya kijeshi kwa kile wanamgambo hao wa itikadi kali walichomwambia kuwa ni "vita vya Jihadi". Kijana huyo anasema alifanikiwa kutoroka, nduguye na kijana mwengine waliokuwa pamoja nae wameuliwa. Baada ya kuishi miaka mitatu katika ncho tofauti za Afrika, amefanikiwa kuingia Ujerumani anakoishi tangu mwaka 2015. Maombi ya Ahmed Muse ya ukimbizi yamekataliwa sawa na yalivyokataliwa maombi ya wenzake kadhaa  kwa hoja Al Shabab hawatokuwa na haja ya kuwasaka wakimbizi wasiokuwa na umuhimu wowote kwa lengo la kuwaadhibu. die Tageszeitung linakumbusha kukataliwa maombi ya ukimbizi , mara nyingi matokeo yake huwa kushinikizwa wahusika kurejeshwa makwao ikiwa wenyewe hawatoridhia. die Tageszeitung linazungumzia maamuzi yanaayotofautiana yanayopitishwa na jimbo moja hadi jengine kuhusiana na hatima ya wakimbizi wa Somalia. Limemaliza kwa kuwanukuu Bernd Mesovic wa shirika la pro Asyl na Luise Amtsberg wa walinzi wa mazingira die Grüne wakikosoa maamuzi ya kuwarejesha wakimbizi wa Somalia nchini mwao.

Mwongezeko mkubwa wa wakaazi wa Afrika unaadhiri maendeleo

Idadi ya watoto wanaozaliwa barani Afrika ni kubwa kupita kiasi. Hali hiyo inahatarisha maendeleo na kusababisha idadi ya wanaolipa kisogo bara hilo kuzidi kuongezeka. Lakini hali hiyo haiwashughulishi hata kidogo watawala wa Afrika  linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine katika ripoti yake iliyoipa jina "Mageuzi Afrika". Baada ya kuzungumzia kuhusu kupungua  hali ya umaskini barani Afrika, gazeti linataja wakati huo huo juu ya kuongezeka idadi ya watu ambao ni maskini barani humo. Chanzo linasema ni ile hali ya kuongezeka kwa kasi kabisa idadi ya wakaazi wa bara hilo ikilinganishwa na jinsi hali ya umaskini inavyopungua. Hakuna nchi yoyote ya dunia ambako idadi ya vijana wasiokuwa na kazi ni kubwa kama Afrika-kinachopatikana kutokana na maendeleo ya kiuchumi kinamezwa na ukuaji mkubwa wa wakaazi wake. Baadhi ya viongozi wa Afrika hawalioni hilo kuwa ni tatizo na hasa wale wa nchi za Afrikia kati na afrika magharibi linaandika gazeti la Frankfurtter Allgemeine lililomnukuu mkurugenzi wa shirika la World Watch, Robert Engelmann.

 Moyo wa subira wa mama Afrika

Ripoti yetu ya mwisho magazetini imeripotiwa na gazeti la Süddeutsche na inamhusu bibi mmoja nchini Uganda maarufu kwa jina  Mama Afrika ingawa jina lake la kweli ni Mariam. Anaishi katika kijiji kimoja cha mkoa wa Kabimbiri mwendo wa saa mbili kwa gari kutoka mji mkuu Kampala. Bibi huyo ana umri wa miaka 37,  lakini anasemekana amezaa watoto 38. Anafanikiwa vipi kuwahudumia watoto hao wote; Mwenyewe anasema anawapa majina watoto kuabatana na tukio lililojiri siku kila mmoja alipozaliwa  kwa namna hiyo hawezi kusahau nani ni nani na pili anasema la muhimu zaidi ni kuhakikisha  hakuna anaependelewa na sio tu na mama mwenyewe bali hata na mashangazi au mashoga mtaani. Watoto wote hao baba yao ni mmoja. Na ingawa kwa muda mrefu amekuwa akiwashughulikia mwenyewe watoto wake, lakini  baada ya gazeti la Daily Mirror kuripoti kuhusu kisa hicho hivi sasa ulimwengu mzima unakifuatilizia na serikali ya Uganda pia imeamua kuingilia kati kumsaidia.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW