1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Rwanda waliokuwa wakiishi Kongo warejeshwa

13 Januari 2022

Wakimbizi wasiopungua 100 raia wa Rwanda waliokuwa wakiishi kinyume cha sheria katika kisiwa cha Idjwi kwa wiki moja huko Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamerejeshwa nchini mwao siku ya Alhamisi.

Symbolbild I Kivu See im Ost Kongo
Picha: Pamela Tulizo/AFP/Getty Images

Watu hao waliwahi kuihama nchi yao wakidai wanaepuka chanjo ya corona inayolazimishwa kwa wakaazi. Wakimbizi waliokuja makundi-makundi, walijihifadhi katika kisiwa hicho cha Idjwi ndani ya Ziwa Kivu tangu zaidi ya wiki moja, wengi wakiwa wa imani ya Waadventista, wakisema kwamba wamekimbia chanjo ya virusi vya corona ambayo wanalazimishwa kuchoma nchini Rwanda.

Mmoja wa raia hao Marie-Gorette Nzayisenga anasema walikuwa wanawatafuta ili wawachome chanjo kwa nguvu- ''Ijapokuwa kwenye hati ya chanjo imeandikwa vyema kuwa chanjo hiyo ni ya hiari. Sasa mamlaka zetu za mitaa zimetutafuta kila mahali kwa nguvu ndiyo maana tumetoroka. Tungependelea kukaa Kongo kuliko kwenda Rwanda. Tunaliomba Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, Shirika la Afya Duniani, WHO na mashirika mengine ya kimataifa kulinda usalama wetu'', alifafanua Nzayisenga.

Kulingana na kiongozi wa jadi katika eneo la ufalme wa Ntambuka ndani ya kisiwa cha Idjwi ya kusini mwami Roger Ntambuka Balekage, jumla ya raia wa Rwanda 101 wamerejeshwa makwao siku ya Alhamisi wakati wa asubuhi, akibainisha kuwa serikali ya mkoa wa Kivu Kusini ilikodisha meli ambayo iliwarejesha.

Roger Ntambuka anaeleza kwamba raia hao wa kigeni walisafirishwa kupitia bandari ya Kashofu nchini Kongo na wamevushwa hadi katika bandari ya Nyamasheke nchini Rwanda.

Amesema kuwa kurejeshwa kwa watu hao kulifanyika kwa ushirikiano kati ya viongozi wa mkoa wa Rubavu nchini Rwanda na Kivu Kusini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na kwamba huduma za uhamiaji za nchi hizo mbili zimejihusisha katika kuwarejesha nyumbani kwa amani na heshima ya haki za kimataifa za kibinadamu.

Esther Muratwa, kiongozi wa shirika la kiraia katika wilaya ya Idjwi amesema ameridhika na shughuli ya kuwarejesha raia hao kwenye nchi yao ya Rwanda.

Wakati huo huo, maafisa wa afya wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wanazidi pia kuwahamasisha wakaazi kuhusu umuhimu wa kupata chanjo dhidi ya janga la virusi vya corona.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW