Wakimbizi wa Syria kurejea nyumbani mwaka ujao
11 Desemba 2018Amin Awad anayesimamia shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR upande wa mashariki ya kati na Afrika ya Kaskazini, aliwaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba wasyria takriban 250,000 wanatarajiwa kurejea nyumbani mwaka 2019, huku akisema idadi hiyo inaweza kuongezeka au kupungua kulingana na kasi ya operesheni hiyo.
Kwa sasa kuna takriban wakimbizi milioni 5.6 wanaoishi katika maeneo wakiwemo wakimbizi milioni 1 waliozaliwa wakati wa vita, hii ikiwa ni kwa mujibu wa data za UNHCR.
Shirika hilo limesema wakimbizi 117,000 wamerejea Syria tangu mwaka 2015 wakiwemo wakimbizi 37,000 mwaka huu.
Licha ya mapigano yanayoonekana kupungua kidogo nchini Syria, mapigano yalioanza mwaka 2011 na kusababisha mauaji ya zaidi ya watu 360,000, Awad amesema wakimbizi wataruhusiwa kurejea Syria kwa hiari na wala sio kwa kulazimisha.
Urusi inasema kurejea kwa wakimbizi Syria kunamaanisha taifa hilo sasa ni shwari
Amin Awad amesema wakimbizi hao huenda wakakabiliwa na pingamizi fulani kuanzia kukosa nyaraka muhimu za kuwatambua pamoja na kutambua mali zao, kukosa elimu, matibabu na usafi wa mahala wanaporejea suala ambalo serikali inapaswa kusaidia katika kulitafutia ufumbuzi.
Huku hayo yakiarifiwa Urusi nayo imesema wakimbizi wa Syria 114,000 wamerejeshwa nyumbani mwaka huu ambayo ni sehemu ndogo ya watu milioni 6 walioitoroka nchi hiyo tangu kuanza kwa mapigano. Kanali generali Mikhail Mizintsev amesema kurejea kwa wakimbizi kunatoa ishara kwamba vita vya Syria vimemalizika na kwamba taifa hilo pole pole linarejea kuwa la kawaida.
Urusi ilioanzisha kampeni ya kijeshi ya kumuunga mkono rais Bashar al Assad imekuwa ikishinikiza raia wa Syria kurejea nyumbani japo serikali za Magharibi zinasema kwa sasa ni mapema mno kuanzisha mchakato huo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mahriri: Josephat Charo