Wakimbizi wafanywa watumwa nchini Libya
15 Agosti 2014Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, waasi wa Libya wanawatumia vibaya wakimbizi kama wanajeshi kuwasaidia katika harakati zao. Shirika la misaada la Italia, Habeshia, limeripoti kwamba waafrika kutoka Eritrea, Somalia, Ethiopia, Mali na Sudan, wanasajiliwa kwa lazima na makundi ya waasi nchini Libya na kutumiwa kusafirisha silaha na hata kutumiwa kama wapiganaji katika uwanja wa vita.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulukia masuala ya wakimbizi, Antonio Guterres, wengi wao tayari wamepata majeraha mabaya au hata kuuwawa katika vita vya Libya ambavyo hawakuvitaka na ambavyo haviwahusu kabisa.
Kwa mitizamo mingi hali ya wahamiaji nchini Libya imekuwa mbaya mno ikilinganishwa na mwaka 2011 baada ya mapinduzi dhidi ya kiongozi wa zamani wa taifa hilo, hayati Muammar Gaddafi. Wakati huo wahamiaji kutoka mataifa ya pembe ya Afrika na kusini mwa jangwa la Sahara, ambao wengi walikwenda Libya kufanya kazi, na kugeuka kuwa wapiganaji wa makundi yaliyomuunga mkono Gaddafi, walifuatiliwa na kutiwa ndani au kufa wakati walipojaribu kuikimbia Libya kupitia bahari ya Mediterania.
Muasisi wa shirika la misaada la Habeshia, padri wa kanisa Katoliki, Don Mussie Zerai, anawasaidia tangu miaka kadhaa wakimbizi waotumia boti kukimbia Libya na ana mawasiliano mazuri na wahamiaji kutoka Afrika kaskazini. Mashirika mengine ya kimataifa yanatumia ujuzi na maarifa yake katika masuala ya wahamiaji.
Misrata ni kubaya kwa wakimbizi
Hali mbaya kabisa ya wakimbizi wa kiafrika nchini Libya imeshuhudiwa mjini Misrata, ambako kwa sasa wakimbizi 700 wengi wao wakitokea Eritrea, wanaume, wanawake na watoto, wamezuiliwa katika eneo linalofanana na kambi ya mateso, ambalo waasi hulitumia kama "ghala la watumwa". Wiki chache zilizopita vijana 225 walichukuliwa kutoka kambini hapo ikisemekana wanapelekwa kazini.
Kupitia vijana saba waliofaulu kurejea kambini ilibainika kuwa vijana hao walishuhudia matukio ya kutisha na wenzao kadhaa waliokuwa pamoja wakiuwawa kwenye mapigano makali. Kufikia sasa inaripotiwa vijana 61 wamerejea katika kambi hiyo.
Wakati wa mapigano ya mwishoni mwa mwezi uliopita na mwanzoni mwa mwezi huu katika mji mkuu Tripoli waasi waliwaburuza vijana kadhaa wahamiaji kutoka majumbani mwao au kuwasaka mabarabarani wakati walipojaribu kuyakimbia mapigano hayo kwenda katika maeneo yaliyo salama.
Shirika la Habeshia limemtaka Guterres na jumuiya ya kimataifa, hususan Umoja wa Ulaya na Marekani, kufanya kila linalowezekana kuwafungulia njia wahamiaji kuondoka nchini Libya kuyanusuru maisha yao. Shirika hilo limesema kwa bahati mbaya taarifa za kwanza kuhusu hali ya wahamiaji nchini Libya wiki mbili zilizopita hazikuibua hisia wala kauli zozote za kisiasa huku utumiaji wa wakimbizi waliogeuzwa kuwa watumwa ukiwa umegeuka kuwa jambo la kawaida nchini humo.
Jumatano wiki hii bunge la Libya liliutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati kuyazima mapigano ya waasi. Bunge hilo lilipiga kura kuyavunjilia mbali makundi yote ya waasi na kuutaka umoja huo kuwalinda raia katika jitihada ya kuyakomesha mapigano kati ya makundi ya waasi wanaohasimiana tangu mapinduzi ya mwaka 2011. Maafisa wa Marekani na Umoja wa Ulaya wana matumaini bunge jipya la Libya litafaulu kuanzisha mdahalo kati ya pande zinazozozana.
Mwandishi: Josephat Charo/Der Tagesspiegel
Mhariri: Saumu Yusuf