1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wauwawa katika shule iliyowahifadhi Gaza

7 Mei 2025

Mashambulizi mapya ya anga ya Israel yamewaua makumi ya raia wa Palestina katika shule zinazowahifadhi wakimbizi wa ndani Gaza.

Gofu la nyumba baada ya shambulizi la Israel
Gofu la nyumba baada ya shambulizi la IsraelPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Haya yanafanyika huku wakosoaji wakilaani mpango wa Israel wa kutaka kudhibiti ugawaji wa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kusitisha mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen, baada ya makubaliano ya kusitisha vita, lakini waasi hao wameapa kuendeleza mashambulizi dhidi ya Israel wakisema wanatetea Wapalestina.

Mashambulizi ya anga ya Israel yamewaua Wapalestina 13 katika shule iliyokuwa ikihifadhi familia za wakimbizi kaskazini mwa Gaza. Shule hiyo, iliyoko Tuffah, Gaza City, ililengwa mara mbili.

Miongoni mwa waliouawa ni mwandishi wa habari Nour Abdu, akifanya idadi ya waandishi waliouawa na Israel kufikia 213 tangu vita kuanza.

Theluthi moja ya Gaza yadhibitiwa na jeshi la Israel

Siku moja kabla, mashambulizi kwenye shule nyingine katikati ya Gaza yaliua watu 29, wakiwemo wanawake na watoto. Jeshi la Israel lilisema lililenga kituo cha kamandi cha Hamas kilichokuwa ndani ya jengo hilo.

Wakati huo huo, operesheni ya kijeshi ya Israel inaendelea kusini mwa Gaza, hasa katika mji wa Rafah, ambapo wanajeshi wanabomoa nyumba na miundombinu.

Jeshi la Israel limedhibiti takriban theluthi moja ya Gaza na kuhamisha maelfu ya watu, wakijenga minara ya ulinzi na vituo vya upelelezi katika maeneo wanayoyaita ya usalama.

Wanajeshi wa IsraelPicha: Israel Defense Forces/Anadolu/picture alliance

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema operesheni hiyo huenda ikapanuliwa hadi kudhibiti Gaza nzima, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa misaada ya kibinadamu kupitia kampuni binafsi.

Israel imesema inatayarisha eneo jipya la kibinadamu karibu na Rafah, ambapo wakimbizi wa ndani watachunguzwa kabla ya kupokea misaada.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yameonya kuwa mkakati huo unaweza kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu (OCHA) ilisema mpango huo ni "kinyume na kile kinachohitajika," huku mashirika mengine yakieleza wasiwasi kuhusu ukosefu wa uwazi na ugumu wa kupeleka misaada.

Huku hayo yakijiri, Marekani imetangaza makubaliano ya kusitisha vita kati ya waasi wa Kihuthi, kwa upatanishi wa Oman.

Makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya Wahuthi.

Kusitishwa mashambulizi Yemen

Rais wa Marekani, Donald Trump, alithibitisha kuwa mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen yamesitishwa baada ya "Wahuthi kusalimu amri” kufuatia wiki saba za mashambulizi ya Marekani.

"Ndio, tumewajulisha tu muda mfupi uliopita, na mashambulizi yote yamekwisha kusitishwa. Wengine huenda bado hawajapata taarifa hii, lakini hadi sasa, tunatarajia kuwa karibu wote wamejulishwa. Tunaamini kwamba mashambulizi yatasitishwa kwa pande zote mbili, na hivyo basi, hali inavyokuwa sasa ndiyo hali halisi," alisema Trump.

Hata hivyo, makubaliano hayo hayaihusishi Israel, na waasi hao wameapa kuendelea kushambulia taifa hilo kwa mshikamano na Wapalestina. Kiongozi wa kisiasa wa waasi hao pia aliahidi kwamba mashambulizi dhidi ya Israel "yataendelea” na yatazidi kile alichokiita "uwezo wa Israel kuvumilia".

Vita vya sasa vya Gaza vilianza Oktoba 7, 2023, baada ya wapiganaji wa Hamas kuua watu 1,200 na kuwateka nyara zaidi ya 250, kwa mujibu wa takwimu za Israel.

Oktoba 7: Jinsi shambulio la Hamas lilivyofanyika

02:23

This browser does not support the video element.

Tangu wakati huo, mashambulizi ya Israel yamewaua Wapalestina zaidi ya 52,000, wengi wao wakiwa raia, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Wakati idadi ya wakimbizi ikiongezeka na misaada ikizuiliwa, mashirika ya kimataifa yanaendelea kuonya kuhusu hatari ya mzozo huo kuongezeka na kusambaa katika maeneo zaidi.

Vyanzo: Reuters/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW