1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wako wapi majenerali wa Urusi? Uvumi waenea baada ya uasi

30 Juni 2023

Majenerali wa ngazi za juu wa Urusi wamepoteza heshma na umahiri wao mbele ya umma baada ya uasi wa Wagner uliolenga kuwapindua wakuu wa jeshi, huku kukiwa na msukumo kwa Rais Vladimir Putin kurejesha mamlaka yake.

Russland Region Primorsky, Vostok | Militärübungen | Wladimir Putin, Präsident | mit u.a. Sergei Schoigu, Verteidigungsminister
Picha: SPUTNIK via REUTERS

Mkuu wa majeshi Jenerali Valery Gerasimov hajaonekana hadharani au kwenye runinga ya serikali, na wala hajatajwa katika taarifa ya wizara ya ulinzi kwa vyombo vya habari tangu Juni 9, baada ya kutibuliwa kwa uasi wakati kiongozi wa mamluki wa Kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin alipotaka Gerasimov akabidhiwe kwao.

Gerasimov, mwenye umri wa miaka 67, ni kamanda wa vita vya Urusi nchini Ukraine,na kulingana na baadhi ya wachambuzi wa kijeshi kutoka matiafa ya Magharibi, kamanda huyo ni mmoja kati ya wamiliki watatu wa "mkoba" wenye siri za nyuklia za Urusi.

Soma pia: Mkuu wa Wagner ahamia Belarus, NATO yaapa kulinda washirika

Mwengine ni Jenerali Sergei Surovikin, aliyepewa jina la utani "Jenerali Armageddon" na vyombo vya habari vya Urusi kwa mbinu yake ya uchokozi katika mzozo wa Syria, ambaye ni naibu kamanda wa Vikosi vya Urusi huko Ukraine.

Ripoti ya New York Times, ilinukuu idara za ujasusi za Marekani kwamba Surovikin alikuwa na taarifa mapema kuhusu uasi wa kundi la Wagner na sasa mamlaka ya Urusi inafuatilia kujua iwapo alishiniriki kwa namna yoyote.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu (kushoto), na mkuu wa majeshi Valery. GerasimovPicha: Sputnik/Aleksey Nikolskyi/Kremlin via REUTERS

Ikulu ya Kremlin ilipuuza ripoti hiyo, ikisema kutakuwa na porojo nyingi na kukakataa kujibu maswali kuhusu Surovikin, na kuwaelekeza waandishi wa habari kwa wizara ya ulinzi ambayo pia bado haijatoa kauli yoyote kumuhusu.

Alipoulizwa kama Putin bado ana imani na Surovikin, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov hakutoa jibu na badala yake alisema tu kwamba Putin alifanya kazi na waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi.

Majenererali walimuunga mkono Prigozhin?

Maafisa wa Marekani waliambia shirika habari la Reuters kwamba Surovikin amekuwa akimuunga mkono Prigozhin, lakini ujasusi wa Magharibi hauna uhakika iwapo aliwasaidia kwa namna yoyote katika uasi.

Soma pia: Je, Prigozhin atakuwa salama nchini Belarus?

Toleo la lugha ya Urusi la Moscow Times na blogu za kijeshi ziliripoti kukamatwa kwa Surovikin, huku waandishi wengine wa habari wa kijeshi wenye wafuatililiaji wengi nchini Urusi walisema kwamba Surovikin na maafisa wengine wakuu walikuwa wakihojiwa na Huduma ya usalama ya FSB ili kuthibitisha uaminifu wao.

Hata hivyo shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha moja kwa moja ikiwa Surovikin na majenerali wengine wamekamatwa au walikuwa wakichunguzwa. Kupitia mtandao wa Telegram Rybar, kituo chenye ushawishi kinachoendeshwa na mwandishi wa habari wa zamani wa wizara ya ulinzi ya Urusi alisema watu watafutwa kazi karibuni.

Urusi inaonesha hali ipo sawa baada ya uasi wa wagner

01:52

This browser does not support the video element.

Taarifa hiyo ilisema mamlaka inajaribu kuwaondoa wanajeshi wanaochukuliwa kuwa wameonyesha "kushindwa kufanya maamuzi" katika kukabiliana na uasi wa mamluki huku kukiwa na ripoti kwamba sehemu fulani ya wanajeshi hawakufanya lolote kuwazuia mamluki wa Wagner katika hatua za mwanzo wa uasi.

Soma pia: Kremlin yasema Putin yupo imara

Na iwapo hatua kama hiyo itathibitishwa, inaweza kubadilisha muelekeo wa Urusi katika vita vyake huko Ukraine ambayo inaiita "operesheni maalum ya kijeshi" na kusababisha msukosuko katika ngazi za jeshi wakati ambapo Moscow inajaribu kuzuia mashambulizi kutoka kwa Ukraine.

Hata hivyo hakukuwa na maoni rasmi kutoka kwa wizara ya ulinzi juu ya kile kinachoendelea. Huku baadhi ya wachambuzi wa kijeshi na kisiasa wa Urusi na Magharibi wanaamini Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu, mshirika mkongwe wa Putin ambaye Prigozhin alitaka kumuangusha pamoja na Gerasimov kwa madai ya uzembe, sasa unaweza kuwa salama zaidi katika kazi yake.

Jenerali Viktor Zolotov, mkuu wa Ulinzi wa Taifa ambaye alikuwa pia mlinzi wa Putin, anaonekana kuwa mnufaika mwingine baada ya kujitokeza hadharani akisema kwamba kikosi chake kilikuwa tayari "kusimama hata kwa kifo" ili kuilinda Moscow kutoka kwa Wagner.

Chanzo: rtrt

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW