1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakongomani wapiga kura leo kuchagua viongozi wapya

20 Desemba 2023

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanajiandaa leo kupiga kura kumchagua rais, wabunge, magavana wa mikoa pamoja na madiwani baada ya muda wa kampeni ya mwezi mmoja kukamilika siku ya Jumatatu.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Uchaguzi Mkuu
Mawakala wa uchaguzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Watu millioni 40 wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi unaoendeshwa wakati mmoja wa rais, bunge, mikoa na manispaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Baada ya mwezi wa mikutano na matamshi makali ya kisiasa, kampeni rasmi ilifikia mwisho usiku wa Jumatatu.

Rais Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60 anawania muhula mwingine wa miaka mitano. Waangalizi wengi wanakubaliana kwamba ana nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi wa leo kutokana na mgawanyiko miongoni mwa wagombea wa upinzani.

Soma pia: Upinzani Kongo wadai kuchezewa ´rafu` kuelekea uchaguzi 

Matatizo ya usafirishaji yanasalia kuwa jambo linalotia wasiwasi mkubwa kuelekea uchaguzi huo, huku kukiwa na wasiwasi kwamba vifaa vya uchaguzi havitafika kwenye vituo vya kura kwa wakati.

Idadi kadhaa ya kadi za wapiga kura pia hazisomeki kutokana na makosa ya uchapishaji, na hivyo kuibua maswali zaidi.

Umoja wa Mataifa ambao umekubali kusaidia kusafirisha vifaa vya uchaguzi, ulikuwa haujapokea maelekezo kutoka tume ya uchaguzi juu ya wapi pa kupeleka vifaa hivyo. 

Kuandaa uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, taifa maskini lenye ukubwa wa Ulaya Magharibi, ni changamoto kubwa ya lojistiki.

CENI: Kumekuwepo mashambulizi ya wadukuzi kwenye mtandao wetu

Wafuasi wa mgombea mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Daktari Denis Mukwege mjini LubumbashiPicha: Paul Lorgerie/DW

Mwenyekiti wa CENI Denis Kadima alisema jana usiku kwamba hana uhakika juu ya iwapo vituo vyote vitafunguliwa kwa wakati, lakini amehakakikisha kuwa watu wote wenye haki ya kupiga kura watatekeleza haki yao, hata ikimaanisha zoezi hilo kwenda hadi siku ya pili.

Kadima alibainisha kuwa CENI imerikodi mashambulizi 3,244 ya wadukuzi kwenye mtandao wake siku ya Jumatatu pekee, na kubainisha kuwa kuna wahalifu wanaojaribu kuvunja mfumo wa tume hiyo, na kuongeza kuwa wamefanikiwa kuwazuwia na kuimarisha mfumo huo.

Soma pia: Mashambulizi ya mitandaoni kwa wagombea urais Kongo 

Hapo jana serikali iliamuru kufungwa kwa mipaka yote ya angani, nchi kavu na bahari kuanzia jana usiku hadi usiku wa Alhamisi. Mkuu wa idara ya uhamiaji ya Kongo, DGM, Roland Kashwantale, alionya kwamba safari za ndani za ndege zimesitishwa isipokuwa safari za kimataifa.

Raia wa DRC wanajiandaa kumchagua rais wao

02:45

This browser does not support the video element.

Katika uchaguzi wa leo, Rais Tshisekedi anakabiliana na wanasiasa kadhaa mashuhuri wa upinzani, akiwemo mfanyabishara mashuhuri, Moise Katumbi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Daktari Denis Mukwege na Martin Fayulu, mgombea alieshindwa na Tshisekedi katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Waangalizi wengi wa uchaguzi huo, likiwemo Kanisa Katoliki, walisema Fayulu ndiye alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo.

Soma pia: Umoja wa Mataifa yakubali kuisaidia Congo katika usafirishaji wa vifaa vya kura

Mwenyekiti wa CENI Denis Kadima amewahimiza wagombea kujiepusha na matamshi ya uchochezi wakati wa kipindi hiki, na kuwahakikishia kwamba matokeo ya uchaguzi yatakuwa yale yalioelezwa na wapiga kura.

Kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa mnamo Disemba 31.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW