Wakristo Ethiopia wamlaumu Abiy kushindwa kuzuwia mauaji
28 Oktoba 2019Kanisa linasema waziri mkuu huyo ameshindwa kuwalinda waumini wa kanisa hilo lenye ushawishi mkubwa nchini Ethiopia.
Ghasia zilizuka katika mji mkuu Addis Ababa na jimbo la karibu la Oromia siku ya Jumatano wiki iliyopita, baada ya mwanaharakati mmoja mashuhuri kuvishutumu vyombo vya usalama kwa kula njama ya mashambulizi dhidi yake, madai ambayo jeshi la polisi limeyakana.
Afisa mmoja wa polisi alisema siku ya Ijumaa kuwa watu 67 waliuwawa katika machafuko hayo katika jimbo la Oromia.
"Watu wanakufa na masuali yanaulizwa endapo kweli serikali ipo. Watu wanapoteza matumaini," alisema kiongozi wa Kanisa la Orthodox la Tawahedo, Baba Markos Gebre-Egziabher, baada ya sala ya kuwaombea wafu kwenye Kanisa la Utatu Mtakarifu mjini Addis Ababa siku ya Jumapili (Oktoba 27).
Wafuasi wa kanisa la Orthodox ni takribani asilimia 40 ya wakaazi wote milioni 110 wa Ethiopia.
Abiy, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu, alitoa kauli yake usiku wa Jumamosi, ambapo aliapa kuwafikisha wahalifu mikononi mwa vyombo vya sheria na kuonya kwamba machafuko yataongezeka ikiwa Waethiopia wasingeliungana.
Msemaji wa kanisa hilo aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waumini 52 wa kanisa hilo, wakiwemo maafisa wawili wa kanisa, ni miogoni mwa waliouawa. Hata hivyo, idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa.