Wakristo kote ulimwenguni waadhimisha Ijumaa Kuu
11 Aprili 2023Papa Francis ataongoza ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baada ya kuwaongoza waumini katika kufuata njia ya Msalaba.
Ijumaa Kuu ni sehemu ya Wiki Takatifu, inayoanza siku ya Jumapili ya Matawi hadi Jumapili ya Pasaka ambapo kulingana na imani ya Wakristo, husherehekea kufufuka kwa Yesu Kristo.
Papa Francis mnamo siku ya Jumamosi iliyopita aliruhusiwa kutoka hospitali moja ya mjini Rome alikokuwa amelazwa kwa ajil ya kutibiwa matatizo ya kifua. Taarifa ya makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican ilisema wakati huo kwamba Baba Mtakatifu atatekeleza ratiba kamili ya Wiki Takatifu, pamoja na ibada ya Ijumaa Kuu pamoja na kushiriki kwenye Misa ya Jumapili katika Uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro.
Mapema jana Alhamisi, Papa Francis aliongoza Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kama sehemu ya miadi yake katika Wiki Takatifu.
Hapa nchini Ujerumani kumekuwepo utamaduni wa watoto kuandika barua na kuelezea hisia zao kupitia kwenye kijiji cha Ostereistedt kilichopo kaskazini mwa Ujerumani. Kwa mujibu wa shirika la Posta wakati huu wa kuadhimisha Ijumaa Kuu barua zipatazo alfu 70 kutoka kwa watoto zimepokelewa.
Mpokeaji barua hizo "Easter Bunny" amesema watoto kutoka sehemu mbalimbali wanataka amani duniani wengine wametaka Chokoleti na hata tiketi za kuingia sinema na mengine mengi. Utamaduni wa kupokea barua za Watoto wakati wa pasaka katika mji wa Ostereistedt ulianza miaka 40 iliyopita.
Chanzo: DPA