1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakristo waanza maadhimisho ya Pasaka

15 Aprili 2022

Licha ya hali ya wasiwasi kutokana na mashambulizi yaliyouwa watu kadhaa ndani ya Israel na Ukingo wa Magharibi, maelfu ya Wakristo wamekusanyika katika mji wa kale wa Jerusalem kuadhimisha Pasaka.

Jerusalem Karfreitagsprozession Christen
Picha: EMMANUEL DUNAND/AFP

Waumini wa Kikristo walibeba misalaba na kufanya matembezi kupitia "Njia ya Msalabani" kuashiria njia aliyopita Yesu Kristo akielekea kusulubiwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Waumini hao baadaye walikusanyika kwenye Kanisa Kuu la Sepulchre, ambako kwa mujibu wa imani ya Kikristo, ndipo Yesu alipokufa na baadaye kufufuka. Hilo ni eneo tukufu kwa Wakristo na ndio kiini cha sherehe zote za Pasaka.

Ijumaa ya leo imekuwa ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitatu kwa watalii na mahujaji kuweza kuingia kwenye eneo hilo kwa ajili ya Pasaka, kutokana na janga la virusi vya korona.

Polisi wa Israel wavamia Msikiti wa Al-Aqsa

Alfajiri ya Ijumaa, polisi wa Israel waliuvamia Msikiti wa Al-Aqsa na kuwajeruhi zaidi ya watu 150 waliokuwamo msikitini humo katika usiku wa kuamkia Ijumaa Kuu ya Pasaka. 

Eneo la Msikiti wa Al-Aqsa ambalo ni takatifu kwa Waislamu na Mayahudi.Picha: Ammar Awad/REUTERS

Msikiti huo ni eneo tukufu kwa Mayahudi na Waislamu na karibu na eneo hilo ndipo lilipo Kanisa Kuu la Sepulchre, lililo takatifu kwa Wakristo.

Polisi walitumia gesi ya machozi na risasi za mpira, kwa mujibu wa shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, huku polisi ikidai kuchukuwa hatua hiyo baada ya watu kuwarushia mawe na kuchoma moto fashifashi.

Polisi ya Israel ilisema inakisia kuwa kulikuwa na wale iliowaita "wafanya fujo" 100 kati ya waumini 12,000 waliokusanyika hapo kwa sala, katika msimu huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Haaretz, polisi, ambao walidai kuwa maafisa wake watatu pia walijeruhiwa, iliwatia nguvuni watu kadhaa kabla ya kuondoka kwenye eneo hilo.

Maelfu ya Waislamu wanatazamiwa kuingia kwenye eneo la Mji Mkongwe wa Jerusalem kuswali Ijumaa ya pili tangu kuanza kwa mfungo wa Ramadhani.

Jioni ya Ijumaa pia ni mwanzo wa sikukuu ya Kiyahudi ya Passover, ambayo ilitamiwa kuwaleta waumini na wageni zaidi. Wizara ya Utalii ya Palestina inatazamia watalii 30,000 wa kigeni kuzuru eneo hilo wiki hii pekee.

Watu 35 wafa ajalini Zimbabwe wakienda Pasaka

Ajali ya basi.Picha: LUTFOR RAHAMAN/bdnews24.com

Nchini Zimbabwe, watu 35 wamefariki dunia na wengine 71 kujeruhiwa wakati basi lililowabeba waumini waliokuwa wakienda kanisani kwa ajili ya ibada ya Pasaka kuserereka na kuangukia bondeni.

Waumini hao wa Kanisa la Kizayuni la Kristo walikuwa wakielekea kwenye mji wa Chipinge ulio kusini mashariki mwa Zimbabwe, wakati ajali hiyo ilipotokea.

Naibu Kamishna wa Polisi wa Zimbabwe, Paul Nyathi, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba chanzo cha ajali ni basi hilo kupakia abiria zaidi ya uwezo wake, kwani nchini Zimbabwe, mabasi ya abiria huruhusiwa kupakia abiria wasiozidi 70. 

Ajali za barabarani ni jambo la kawaida nchini Zimbabwe wakati wa sikukuu, ambapo barabara huwa zimejaa magari na watumiaji wengine. Barabara nyingi zina mashimo, jambo linalochangia ajali hizo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW