1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Hawa Bihoga3 Oktoba 2018

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na wakulima wengi kukata tamaa.

Initiative Seeds for Needs
Picha: Bioversity International/C. Fadda

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na wakulima wengi kukata tamaa ya kulima mazao ya chakula kwa kile walichokitaja kuwa soko kutokuwa la uhakika, huku wakishuhudia anguko kubwa la bei ya mazao ya chakula. 

Mwenyekiti wa mtandao wa wakulima wadogo Mviwata Abdul Gea akiwasilisha mawazo ya wakulima wadogo mbele ya Waziri mkuu Kassimu Majaliwa amesema huenda nchi ikakumbwa na baa la njaa kutokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika kwa miaka mitatu mfululizo, licha ya mkulima kuzalisha mazao kwa wingi kama wanavyosisitizwa na serikali.

Hata hivyo licha ya mkulima mdogo nchini Tanzania kuwa na mchango mkubwa wakati taifa likipitia vipindi vigumu kwa nyakati tofauti, ikiwemo wakati wa kupata uhuru na vita ya kagera, na kutajwa kusimama imara kuhakikisha taifa linaondoa dosari ya njaa kwa kuchangia chakula kwa asilimia tisini, wanasema bado hakujawa na mipango imara na yenye tija kwa kundi hilo la wakulima.

Hili linalifanya shirika la chakula ulimwenguni FAO kutoa sisitizo la wakulima kuhakikisha wanaendelea kutekeleza jukumu lao la kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi ili kuwe na dunia ambayo hakuna njaa.

Akitoa msimamo wa serikali katika kushughulikia changamoto za wakulima ikiwemo masuala ya soko, waziri mkuu Kaasim Majaliwa amesema kuwa tayari nchi imeshafanya mazungumzo na mataifa yaliooendelea kama China, Japan na hata ujerumani kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika, ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kama vile muhogo.

Wakulima wasema bado hakujawa na mipango imara na yenye tija kwa wakulima wadogoPicha: Imago

maadhimisho haya yatafatiwa na kongamano la wakulima litakalo wajumuisha wakulima, wakurugenzi wa benki, maafisa wa ngazi mbalimbali serikalini na watajadili kwa uwazi changamoto za mkulima shambani ili kuleta uhalisia katika kauli ya kilimo ni uti wa mgongo wa taifa na baadae kuja na mapendekezo ambayo serikali pamoja na wadau wa kilimo wanapaswa kuyatekeleza.

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW