Wakulima waandamana tena Ulaya
29 Januari 2024Usiku wa kuamkia Jumatatu (Januari 29), wakulima waliendesha matrekta, mabuldoza na magari mengine yanayotumika kwenye shughuli za kilimo mashambani kuelekea mjini Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji na yaliko makao makuu ya Umoja wa Ulaya.
Lengo la wakulima hao lilikuwan ni kuzifunga barabara kuu, lakini wakisema hawakutaka kabisa kuvuruga shughuli za raia wa kawaida kama vile huduma za maduka, matibabu na masomo.
Matrekta mengine yalifika hadi kwenye Kasri Kuu la Luxembourg kwenye kitovu kabisa cha mji wa Brussels.
Wakulima wa Ufaransa waapa kuizingira Paris
Hali kama hiyo ilishuhudiwa pia nchini Ufaransa, ambako wakulima wamezifunga njia kuu kuelekea, Paris, kwa kile wanachokiita "mzingiro wa mji mkuu" huo.
Mkuu wa Muungano wa Wakulima (FDSEA), Regis Desrumaux, aliapa kwamba wangeliendelea na maandamano yao licha ya Waziri Mkuu wa Ufaransa, Gabriel Attal, kutuma maafisa usalama 1,500 kukabiliana na mzingiro huo.
Soma zaidi: Wakulima wa Ujerumani waandamana nje ya ukumbi wa maonyesho ya Wiki ya Kimataifa ya Kijani
"Kwa hali yoyote ile, sisi tunasonga mbele na maandamano yetu. Leo tupo hapa. Tunaiacha barabara kuu kwa mara ya kwanza ndani ya takribani siku nane. Tunachukuwa barabara ya RN 31, na jioni ya leo tumeamuwa kurejea hapa. Ndiyo hivyo, tunasogea mbele kidogo na tunazidi kuongezeka, na tutaendelea." Alisema mkuu huyo wa wakulima wa Ufaransa.
Serikali ya Ufaransa imesema inaachana na mipango yake ya kupunguza ruzuku za kilimo, mafuta ya dizeli na kuahidi kulegeza sheria zinazoibana sekta hiyo, lakini vyama vya wakulima vinasema havijaridhishwa na ahadi hizo.
Wakulima wa Ujerumani waifunga bandari ya Hamburg
Maandamano kama hayo yalishuhudiwa pia nchini Ujerumani, ambako wakulima walitumia matrekta kuzifunga njia zinazoingia na kutokea kwenye bandari muhimu.
Matrekta 100 yaliegeshwa kuelekea bandari kubwa ya Hamburg, na kutiribua usafirishaji wa makontena kwenye bandari hiyo ambayo ni mojawapo ya bandari kubwa kabisa barani Ulaya.
Soma zaidi: Ujerumani yawaambia wakulima wanaoandamana 'hakuna fedha'
Polisi ilisema kwa ujumla matrekta 1,500 yameshiriki kwenye maandamano ya leo kote mjini Hamburg.
Bandari nyengine katika pwani ya kaskazini, kama vile Wilhelmshaven na Bremerhaven, nazo pia zilikumbwa na kadhia hiyo.
Polisi ilisema ilifanya mazungumzo na wakulima hao ili waruhusu kazi iendelee kwenye bandari ya Bremerhaven.
Wakulima nchini Ujerumani wamekuwa wakiandamana tangu mwezi Disemba kupinga mipango ya Kansela Olaf Scholz kuondosha ruzuku kwenye sekta ya kilimo baada ya hukumu ya mahakama kuonesha mapungufu makubwa kwenye mipango ya matumizi ya serikali.
Hata baada ya serikali kuachana kwa sehemu fulani na mipango yake ya kukata ruzuku, na kuahidi kurejesha punguzo kwenye kodi ya vyombo vya usafiri sambamba na kurefusha muda wa kuondosha ruzuku ya mafuta ya dizeli, bado vyama vya wakulima vimeendelea na maandamano yao, vikiitaka serikali kuachana kabisa na mipango ya kuondosha ruzuku.
Vyanzo: Reuters, AFP