Wakurdi wa Iraq wateremka vituoni kulichagua bunge jipya
30 Septemba 2018Matokeo yanatarajiwa kutangazwa masaa 72 baadae. Wadadisi wanasema matokeo hayo yatashawishi zoezi la kuchaguliwa rais wa shirikisho na bunge la nchi hiyo kesho jumatatu mjini Baghdad, wadhifa ambao kijadi hudhibitiwa na Mkurd.
Hadi saa 12 jioni, wapiga kura milioni tatu na laki moja watawachagua wabunge 111 kati ya wagombea 673 wanaowakilisha vyama 29 vya kisiasa- viti 11 vinatengwa kwaajili ya jamii za wachache na za kidini za Waturkmenia, Wakristo na Waarmenia.
Jimbo la kaskazini mwa Iraq wanakoishi jamii kubwa ya Wakurd lina mikoa mitatu na limejipatia utawala mkubwa wa ndani tangu mwaka 1991. Hivi sasa lakini viongozi wa jimbo hilo wanalazimika kujadiliana na serikali kuu ya mjini Baghdad iliyoyamwagia mchanga matumaini yao ya kuwa huru.
September mwaka 2017 wakurd walikwenda kinyume na msimamo wa serikali ya Baghdad na jumuia ya kimataifa na kupiga kura kwa wingi mkubwa ya kutaka kujitenga. Serikali kuu ilikasirishwa na matokeo yake yakawa kuyadhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakishindaniwa na zaidi kuliko yote kudhibiti mapato muhimu yanayotokana na mafuta.
Ndoto ya kuwa huru imetoweka
Ndoto ya kuwa na taifa huru imetoweka. Viongozi wa mjini Erbil wamepoteza madaraka ya kuuza mapipa 550.000 ya mafuta kwa siku na hivi sasa wanapokea asilimia 12 ya fedha kutoka serikali kuu - kiwango ambacho ni sawa na dala bilioni moja kwa mwezi. Hata hivyo kiwango hicho ni haba kuweza kufidia nakisi ya bajeti katika eneo ambalo uchumi wake unategemea mapato ya mafuta na kukabwa na watumishi wa serikali wasiokuwa na idadi.
Zaidi ya hayo mapambano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali yameigharimu fedha nyingi pia serikali kuu sawa na jimbo la kaskazini mwa Iraq na kulitumbukiza katika vurugu jimbo hilo kwa muda wa miaka mitatu."Viongozi wepya wanabidi wayashughulikie zaidi matatizo ya wananchi na hasa watu maskini", anasema Soran Rassoul mkaazi wa Souleimaniyeh ambae hana kazi.
Kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya wafuasi wa Jalal Talabani na wale wa Massud Barzani
Uchaguzi wa mwaka huu una umuhimu mkubwa kwasababu unafanyika siku moja kabla ya wabunge mjini Baghdad kumchagua rais wa jamhuri ya Iraq.
Wadhifa huo hadi wakati huu alikuwa akikabidhiwa mgombea wa chama cha Umoja wa Wazalendo wa Kurdistan PUK cha rais wa zamani wa Iraq, marehemu Jalal Talabani. Kesho lakini na kwa mara ya kwanza chama cha Demokrasia ya Kurdistan cha Massud Barzani-KDP kitagombea pia wadhifa huo.
Chama cha KDP kinadhibiti viti 38 katika bunge huku mpinzani wake mkubnwa chama cha PUK kikikalia viti 18. Chama kikuu cha upinzani Goran (Mageuzi) kinakalia viti 24 katika bunge linalomaliza mhula wake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Yusra Buwayhid