1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa Afrika Mashariki wakubali kupeleka jeshi, DRC

21 Juni 2022

Wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki wamekubaliana jana Jumatatu kupeleka jeshi la kikanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kujaribu kumaliza vita mashariki mwa nchi hiyo.

EAC Staaten Video-Konferenz |  Uhuru Kenyatta
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Wakuu wa mataifa ya Afrika Masharikipamoja na kukubaliana kuanzisha jeshi hilo, wametoa pia mwito wa kusimamishwa mapigano mara moja. Wakuu hao walikutana jijini Nairobi kujadili hali ya usalama kwenye eneo hilo. 

Hatua hiyo imetangazwa na ofisi ya rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta baada ya wakuu wa mataifa saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya mazungumzo kuhusiana na kuongezeka kwa machafuko katika eneo hilo tete. ambayo pia yanatishia hali kwenye mataifa jirani.

Sehemu ya taarifa hiyo imesema wakuu hao wameliagiza jeshi hilo la kikanda kwa kushirikiana na vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kurejesha utulivu na kuhakikisha amani nchini humo. Wakuu hao aidha, wameagiza kusimamishwa mapigano lakini pia kuondolewa kwa uhasama mara moja.

Rwanda inahusishwa?

Hata hivyo taarifa hiyo haikusema chochote kuhusiana na iwapo wanajeshi kutoka Rwanda watahusishwa kwenye jeshi hilo la kikanda, ingawa tayari serikali ya Kongo inasisitiza kwamba hawataki kuona wanajeshi hao wakijumuishwa.

Sehemu ya taarifa ya ofisi ya rais wa DRC, Felix Tshisekedi imesema jeshi hilo linatakiwa kuanza operesheni zake katika kipindi cha wiki zijazo, na lisijumuishe chochote kutoka jeshi la Rwanda.

Mvutano ni mkubwa kati ya rais wa DRC, Felix Tshiekedi na Paul Kagame wa Rwanda kutokana na kushutumiana kuchochea vita.

Marais wa Rwanda Paul Kagame na Felix Tshisekedi walihudhuria mazungumzo hayo ya Nairobi yaliyoandaliwa na rais Kenyatta. Pamoja nao ni wakuu wa mataifa ya Burundi, Sudan Kusini na Uganda, pamoja na Tanzania iliyowakilishwa na balozi wake nchini Kenya. Kagame alihudhuria, licha ya Rwanda kuwa mwenyeji wa mkutano unaowakutanisha wakuu wa serikali za Jumuiya Madola kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni, CHOGM, baadae wiki hii.

Soma Zaidi: Rais Tshisekedi asema Rwanda inaendesha "vita ya kiuchumi"

Mkuu wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmat ameyakaribisha matokeo ya mazungumzo hayo katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa twitter. Imemnukuu akisema anaomba utekelezwaji wa haraka wa maamuzi hayo ili kurejesha amani mashariki mwa Kongo.     

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini inapambana kuyadhibiti makundi ya wanamgambo waliojihami kwa silaha mashariki mwa taifa hilo, na mengi miongoni mwao yakiwa yametokana na vita viwili vya kikanda vilivyodumu kwa robo muongo uliopita.

Mapigano makali yaliyozuka hivi karibuni huko mashariki yamefufua uhasama wa muda mrefu kati ya Kinshasa na Kigali huku DRC ikiimlaumu jirani yake Rwanda kwa kurejea kwa kundi la waasi wa M23. Hata hivyo Rwanda imekuwa ikikana kuwasaidia waasi hao, huku mataifa hayo kwa pamoja yakishutumiana kwa kufanya mashambulizi yanayovuka mipaka.

Soma Zaidi: Mvutano kati ya Congo na Rwanda wapamba moto

Mashirika: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW