1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa jeshi wakamatwa kwa mapinduzi Sudan

Faiz Musa25 Julai 2019

Baraza la Mpito la Kijeshi nchini Sudan limetangaza kuwakamata baadhi ya wakuu wa jeshi pamoja na wanajeshi wengine waliohusika katika jaribio la mapinduzi lililofeli wiki mbili zilizopita.

Sudan | Militärregierung PK Putschversuch  vereitelt
Picha: picture-alliance/AA

Baraza hilo la mpito lilieleza kwamba wanajeshi hao walikuwa na mpango wa kukirudisha tena mamlakani chama cha aliyekuwa rais wa nchi Omar Al Bashir aliyepinduliwa mapema mwezi Aprili cha National Congress. Mkuu mpya wa majeshi, Jenerali Mohammed Othman A-Hussein alitangaza kupitia televisheni ya serikali, kwamba njama ya mapinduzi hayo ilikuwa ni kukirudisha madarakani chama hicho na kuzuia kupatikana kwa suluhu ya kisiasa ya kuweka serikali ya kiraia.

"Watu waliohusika wakiongozwa na Generali Hashem Abdel-Muttalib Babakr na maafisa wengine wakuu  katika jeshi na idara ya ujasusi na idara nyengine za ulinzi na viongozi wa vuguvugu la Kiisilamu wakiwemo na wakuu wa chama cha National congress walikamatwa na uchunguzi unaendelea ili kuweza kuwafungulia mashtaka," alisema Othman.

Vuguvugu la Kiisilamu lilitoa taarifa yake likikanusha kuhusika katika jaribio hilo la mapinduzi. Miongoni mwa wengine waliokamatwa ni aliyekuwa makamu wa rais na waziri mkuu katika mapinduzi yaliyomuweka madarakani Omar Al Bashir mwaka 1989, Generali Bakri Hassan Saleh, mwengine ni aliyekuwa waziri wa masuala ya kigeni Ali Karty na aliyekuwa waziri wa fedha Zubair Ahemd Hassan

Raia wa Susdan akipita karibu na bango la chama cha Nationa Congress, 2015Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Julai 11 Baraza la Mpito lilitangaza kwamba walifanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi japo hawakutoa maelezo ya wapi hasa mapinduzi hayo yalikuwa yatokee. Lilieleza kwamba kwa majuma kadhaa wamekuwa wakifuatilia njama za mapinduzi na tayari maafisa 12 walikuwa wamekamatwa wakiwemo maafisa watano ambao ni wastaafu.

Mazungumzo ya serikali ya kiraia yanaendelea

Professa Hamid Eltgani Ali katika chuo kikuu cha Marekani mjini Cairo, ametilia shaka uwepo wa jaribio la mapinduzi na kusema kwamba kilichopo ni kwamba Baraza la Mpito limebuni jambo hilo kwa lengo la kujiimarisha na kujipa nguvu zaidi kimadaraka.

Baraza hilo la Mpito la Sudan linaendelea na mazungumzo na viongozi wa makundi yaliyofanya maandamana kumtoa Bashir mamlakani pamoja na viongozi wa upinzani kutengeneza makubaliano ya serikali ya mpito itakayohudumu kwa muda wa miaka mitatu kabla ya uchagzi mkuu kufanywa.

Mchakato huo umekuwa ukikwama mara kwa mara na kikao chengine kinatarajiwa Jumamosi wiki hii. Pande zote bado hazijakubaliana kuhusu maswala mengine muhimu kama vile haki kwa wananchi waliouliwa katika miezi ya maandamano.

(DPAE/AFPE/RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW