1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa majeshi wa Uganda na Kongo wakutana Beni

John Kanyunyu6 Aprili 2023

Wakuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda wanakutana mjini Beni ili kutathmini operesheni za pamoja dhidi ya kundi la kigaidi ADF huku wanachi wakisubiri kwa hamu matokeo ya kikao hicho.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo I Wanajeshi wa Uganda na Kongo
Wanajeshi wa Uganda na Kongo katika operesheni ya pamoja ya kijeshi dhidi ya makundi ya waasi huko Beni mwaka 2021Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Wakizungumza na DW katika mitaa ya Beni, wakaazi tuliokutana nao walisema kwamba walisubiri kwa muda mrefu kikao kikubwa kama hiki kufanyika katika eneo lao, wakiwa ni wahanga wa mauwaji yanayofanywa na kundi la kigaidi kutoka Uganda, Alliance Democratic Forces - ADF.

Raia wa Beni, Irumu na Mambasa wanasubiri kwa hamu sana operesheni za pamoja kati ya jeshi la Kongo, FARDC, na lile la Uganda, UPDF, kuanzishwa katika maeneo ya magharibi, walikokimbilia baadhi ya makamanda wa ADF pamoja na idadi kubwa ya wapiganaji wao.

Wanajeshi wa jeshi la Kongo FARDC wakiwa kwenye gari la kijeshi huko Kivu KaskaziniPicha: Alain Wandimoyi/AFP

Nayo mashirika ya kiraia yakiwa yanatambua na kuona mafanikio ambayo ya operesheni hizo, baada ya kuuawa kwa baadhi ya makamanda muhimu wa ADF, yanaomba operesheni hizo kuenea katika maeno yote hapa, ili kuhakikisha kwamba kundi la ADF linatokomezwa na amani ya kudumu inarudi katika maeneo haya, yanayoshuhudia mauaji, tangu Oktoba mwaka wa elfu mbili na kumi na nne.

Msemaji wa majeshi ya muungano Luteni Kanali Mak Hazukay anasema kuwa kikao cha leo kinatuama katika suala hilo na awamu ya tano ya operesheni zenyewe huenda itapelekea majeshi kutumwa magharibi ya Beni.

"Tutaona uwezekano wa kueneza operesheni za pamoja katika maeneo ambayo vikosi vya pamoja vilikuwa bado havijapelekwa huko."

Tujulishe kwamba,  wanajeshi wa Uganda walivuuka mpaka kuingia Kongo Novemba mwaka wa elfu mbili na ishinini kuungana na wenzao wa Kongo kuwatokomeza wapiganaji wa ADF, ambao wamekuwa wakiwauwa watu na kuteketeza mali ya raia wa Beni, Irumu na Mambasa, tangu mwaka wa elfu mbili na kumi na nne. Hadi sasa, maelfu ya raia wameshauawa na kundi hilo la kigaidi.