1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi kuanza kuhutubia mkutano wa UNGA wiki ijayo

19 Septemba 2025

Zaidi ya wakuu wa mataifa 140 ulimwenguni watakuwepo mjini New York wiki ijayo kwa ajili ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaogubikwa na masuala yanayohusu Palestina, ingawa Rais wa Palestina hatakuwepo.

Marekani New York 2024 | Benjamin Netanyahu akihutubia Kikao cha 79. cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza wakati wa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 27, 2024Picha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Lakini wakati masuala haya ya Palestina yakitarajiwa kuchukua nafasi kubwa, kiongozi mmoja na muhimu hatakuwepo, naye ni Mahmud Abbas, rais wa Mamlaka ya Palestina. 

Mkutano huu wa kilele utaanza siku ya Jumatatu, ukiongozwa na Saudi Arabia na Ufaransa ukiangazia mwelekeo wa suluhu ya mataifa mawili ya Israel na Palestina itakayoruhusu mataifa yote hayo kuwa na nafasi kwenye makubaliano ya amani baina yao.

Baada ya Baraza Kuu wiki iliyopita kuidhinisha kwa wingi waraka unaounga mkono mustakabali wa Taifa la  Palestina -- bila ya Hamas -- kwenye mkutano huu kunatarajiwa kushuhudia kutambuliwa rasmi kwa taifa la Palestina na nchi kadhaa, hasa Ufaransa.

Hata hivyo, Rais mmoja atashindwa kuhudhuria licha ya kuhusika moja kwa moja kwenye suala hili. Mahmud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Palestina alinyimwa visa ya kuingia nchini Marekani kushiriki mkutano huo sambamba na maafisa wa serikali yake.

Wapalestina kutoka Gaza City wanaelekea kusini na mali zao, wakipita kwenye barabara ya pwani karibu na kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza, Septemba 19, 2025Picha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

Wachambuzi waonya ikiwa Israel itataka kujibu "mapigo"

Richard Gowan, mchambuzi kutoka Kundi linalofuatilia mizozo la Crisis Group, ameitaja hatua hii kama "ishara" inayoweza kuwa na umuhimu mkubwa "ikiwa nchi zinazoitambua Palestina zitachukua hatua zaidi za kujaribu kuiwekea shinikizo Israel ili kumaliza operesheni zake huko Gaza, ingawa ametahadharisha, ikiwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel atataka kujibu mapigo na hatari ya "kuongezeka" kwa mzozo.

Netanyahu anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu na tayari amekwishasema hakutawahi kuwa na taifa la Palestina chini yake. Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa Israel imepinga kutambuliwa kwa Palestina kama dola huru, na kuapa kuwanyima visa ujumbe wa Palestina akiwemo Abbas.

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Palestina, akihudhuria Mkutano Mkuu wa 79 (UNGA) katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, NY, Septemba 24, 2024Picha: Anthony Behar/Sipa USA/picture alliance

Baraza hilo litapiga kura siku ya Ijumaa ili kumruhusu rais wa Palestina kuzungumza kwa njia ya video. Macho na masikio yatakuwa kwa Rais wa Marekani Donald Trump wakati Abbas atakapozungumza kwenye mkusanyiko huo, ambao kwa kiasi kikubwa husimamisha shughuli katika mji wa Manhattan kila mwaka huku msafara wa magari na wasindikizaji waliojihami kwa silaha nzito wakikagua mtaa wa First Avenue, uliko Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Miaka miwili tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas katika eneo la Ukanda wa Gaza, vilivyochochewa na shambulizi la Hamas nchini Israel, Oktoba 23, 2023, mzozo mkubwa wa kibinaadamu unaoshuhudiwa kwenye ardhi hiyo ndogo ya Palestina, utagubika kusanyiko hilo la ngazi za juu.

Tangu aliporejea madarakani, Rais Trump alianza kupunguza kwa kiasi kikubwa msaada wa Marekani, na kuzorotesha pakubwa utoaji wa huduma wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa misaada, katikati ya ongezeko la mahitaji. Katikati ya mzozo mkubwa wa kifedha na vita vya kila upande, Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 80 kimya kimya huku ukijitetea dhidi ya ukosoaji juu ya ufanisi wake.

Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa akizungumza wakati wa uundaji wa Baraza la Mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Syria, huko Damascus, Syria Machi 29, 2025.Picha: Khalil Ashawi/REUTERS

Rais Al-Sharaa kuhutubia UNGA kwa mara ya kwanza

Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa atakuwa kiongozi mpya na maarufu kwenye kundi hili la wakuu 140 wa mataifa, ambao ni pamoja na Rais Volodymyr zelensky wa Ukraine, Luis Inacio Lula da Silva wa Brazil na Masoud Pezeshkian wa Iran.

Macho yote sasa yatakuwa kwa Sharaa ambaye atahutubia kusanyiko hilo baada ya karibu mwaka mmoja wa kumuondosha Bashar al-Assad na sasa akijaribu kukabiliana na changamoto za kujenga upya nchi hiyo baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mipango ya nyuklia ya Iran nayo itakuwa ni ajenda muhimu, huku kukiwa na wasiwasi wa vikwazo dhidi yake vilivyoondolewa miaka kumi iliyopita kurejeshwa upya mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba, kufuatia mchakato ulioanzishwa mwezi Agosti na Paris, London na Berlin.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na Rais Lula pia wataratibu mkutano wa kilele wa masuala ya hali ya hewa siku ya Jumatano, ambako mataifa kadhaa huenda yakatangaza malengo mapya ya kupunguza gesi chafu, wiki kadhaa kabla ya mkutano wa mazingira wa COP30, nchini Brazil.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW