Wakuu wa Ulaya wakutana kupanga mkakati wa siku za usoni
9 Mei 2019
Viongozi wa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya, isipokuwa Theresa May, waziri mkuu wa Uingereza ambayo inatarajiwa kuondoka, wanakutana katika mji wa Sibiu, nyumbani kwa rais wa Romania ambaye ni mwenyeji wao. Viongozi hao wanatarajiwa kujaribu kuonyesha mshikamano katika msukosuko uliosababishwa na mchakato wa Uingereza kujiondoa, maarufu kama Brexit.
Soma Zaidi: Mchakato wa Brexit wacheleweshwa miezi sita
Umoja huo pia unaandamwa na kitisho cha migawanyiko huku uchaguzi muhimu wa bunge la Ulaya ukipangwa kufanyika katika muda wa majuma mawili. Migawanyiko hiyo inadhihirika hususan katika sera ya uhamiaji, mwelekeo sahihi wa kidemokrasia wakati vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vikiendelea kupata umaarufu, na katika mahusiano na nchi kubwa kama Marekani, Urusi na China.
Mafanikio yaliyoiunganisha Ulaya yenye uhuru na amani
Kiongozi wa Chama cha Watu wa Ulaya katika bunge la Umoja wa Ulaya -EPP, Manfred Weber kutoka Ujerumani ambaye anashiriki katika mkutano huo, amesema umoja huo umekuwa wenye manufaa makubwa na kwamba hauwezi kuachiwa utetereke.
''Kwa umri wa miaka 46, niko katika kizazi cha kwanza cha watu wa Ulaya wanaoweza kusema tunaweza kuishi kokote barani humu kwa amani na uhuru. Haya ni mafanikio makubwa sana, ambayo tunayaonea fahari.'' amesema Weber, na kuongeza kuwa EPP ilikuwa nguzo muhimu ya mafanikio haya, na ni sehemu ya waasisi wa Ulaya yetu hii.
Soma zaidi: Homa ya uchaguzi wa bunge la Ulaya yapanda
Manfred Weber ni miongoni mwa watu waliopendekezwa na bunge la Ulaya katika uongozi wa kamisheni ya Ulaya, kuchukua nafasi ya mwenyekiti wake anayeondoka Jean Claude Juncker. Uongozi wa kamisheni hiyo, pamoja na nafasi nyingine muhimu nne katika Umoja wa Ulaya, utajadiliwa ingawa kwa mchakato usio rasmi. Nafasi hizo nne ni rais wa Halmashauri ya Ulaya, spika wa bunge la Ulaya, mkuu wa benki ya Ulaya na mkuu wa diplomasia wa umoja huo.
Mafungamano katika shida na furaha
Kulingana na rasimu la maazimio ya mkutano huo wa kilele ambayo shirika la habari la Reuters limepata nakala yake, viongozi hao watasaini azimio la ahadi ya kulinda umoja ndani ya Ulaya katika nyakati za neema na za matatizo, na kufanya juhudi mara zote kupata suluhisho linalokubaliwa na wote.
Yanajadiliwa pia malengo ya kimkakati katika kipindi cha kati ya mwaka 2019-2024, ambayo ni kuzidisha ushirikiano katika ukanda unaotumia sarafu ya euro, maendeleo katika kuunda ''akili ya kubuni'' kwa maana ya mashine zinazojiendesha, na kuhamia katika matumizi ya nishati endelevu na rafiki kwa mazingira. Hata hivyo hakuna maamuzi ya mwisho yatakayochukuliwa katika mkutano huu kuhusiana na malengo hayo.
ape,rtre
.