Wakuu wa ulinzi wakutana Paris kujadili IS
20 Januari 2016Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carted ameuelezea mkutano huo, kama nafasi murua ya washirika wakubwa dhidi ya kundi la IS, kubadilishana mawazo juu ya jinsi ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya kundi hilo. Pamoja na Marekani, nchi nyingine zinazoshiriki ni Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Italia. Australia na Uholanzi pia zimealikwa katika mkutano huo
Waziri Carter amesema yeye na wenzake watajadili njia za kusogeza mbele mapambano, kwa kutazama uwezo walio nao kijeshi, ma mahitaji waliyo nayo kuweza kutekeleza mipango yao.
Afisa mmoja kutoka Ufaransa, nchi ambayo ilikuwa ya kwanza kujiunga na Marekani katika operesheni dhidi ya IS, amesema kilicjho muhimu sio kuongeza idadi ya ndege zinazotumiwa katika operesheni hizo, bali pia kuyapa uwezo makundi katika nchi ilipo IS, ili yaweze kulinyang'anya kundi hilo maeneo linayoyadhibiti.
Canada, Urusi zatengwa
Canada, ambayo waziri wake mkuu mpya Justin Trudeau ameapa kuziondoa ndege za nchi yake katika operesheni dhidi ya IS, imetengwa katika mkutano huo, kama ilivyo Urusi ambayo Ufaransa ilikuwa inatakwa pia ishirikishwe.
Na katika ishara ambayo inatazamwa na wachambuzi kama yenye umuhimu mkubwa, hakuna nchi yoyote ya kiarabu iliyoalikwa kushiriuki katika mkutano huo wa Paris. Afisa mmoja wa wizara ya Ulinzi ya Marekani, amesema nchi nyingi za kiarabu kwa wakati huu zinajishughulisha zaidi na operesheni zinazoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wahouthi nchini Yemen.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema katika mkutano wa leo wataangalia namna ya kuzishirikisha zaidi nchi za kiislamu zenye wasuni wengi, ambao hawapendezwi na namna Marekani inavyosaidia serikali ya Iraq ambayo inadhibitiwa na washia.
''Nataka kupata maoni ya washirika wetu kuhusu suala hilo, kwamba nchi za kiarabu zenye wasuni wengi zinapaswa kuchangia ipaswavyo katika operesheni hizi'', amesema waziri huyo wa ulinzi wa Marekani, Ashton Carter.
Siasa za ndani ya Marekani
Warepublican nchini Marekani wanafanya chini juu kuonyesha kwamba mkakati wa rais Barack Obama dhidi ya kundi la IS umeshindwa, wakitaja uwezo wa kundi hilo kuendelea kufanya mashambulizi ya umwagaji damu katika nchi zilizo mbali na ngome zake.
Lakini Waziri Carter amejaribu kuonyesha sura tofauti, kwa kuzingatia mafanikio ya jeshi la Iraq dhidi ya wanamgambo hao, hususan ushindi wa hivi karibuni mbao ulilifurusha kundi la IS kutoka mji muhimu wa Ramadi.
Pia, ameangazia juhudi zinazopangwa kulisambaratisha kundi hilo katika mji wa Raqqa nchini Syria, na Mosul nchini Iraq.
Afisa wa Ufaransa ingawa lipo shinikizo kutaka mashambulizi ya anga dhidi ya IS yaongezwe, operesheni yao inayoongozwa na Marekani inatatizwa na umakini katika kuepuka kuwauwa raia.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo