1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Wakuu wa EU wakutana Brussels mara ya mwisho kwa mwaka 2024

20 Desemba 2024

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wame mjini Brussels kujadili masualaa kadhaa muhimu, ikiwemo msaada kwa Ukraine, upanuzi wa umoja huo pamoja na kufikia uamuzi juu ya kujihusisha na utawala mpya nchini Syria.

Ubelgiji Brüssels 2024 | Rais Zelensky
Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari baada ya kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Disemba 20, 2024Picha: John Thys/AFP

Mkutano wa kilele mjini Brussels ni wa mwisho kwa viongozi wa Umoja wa Ulayakwa mwaka huu wa 2024. Masuala yaliyotiliwa kipaumbele kwenye kusanyiko hili ni vita vya nchini Ukraine, Syria na masuala mengine muhimu.

Viongozi hawa wamekutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kujadiliana naye kuhusu hali ilivyo nchini mwake na matarajio kuhusu mazungumzo na Urusi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya hata hivyo walisisitiza kwamba hakutakuwepo na maamuzi yatakayochukuliwa kuhusu mustakabali wa taifa hilo lililoharibiwa na vita, bila ya kibali kutoka kwa Ukraine ama kuungwa mkono na washirika wake wa Ulaya, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja, hadi Rais mpya wa Marekani Donald Trump atakapoingia madarakani.

Soma pia:Viongozi wa mataifa ya Ulaya na NATO kuijadili Ukraine 

Zelensky asema anaamini ataweza kushirikiana na Trump 

Rais wa Ukraine mwenyewe, Volodymyr Zelensky amesema hapo jana mjini Brussels kwamba anamjua Trump kuwa ni mtu thabiti na anatamani sana awe upande wake.

Alisema "Karibu, Donald! Niseme nini? Kwetu, ni muhimu sana.. Nadhani Rais Trump ni mtu thabiti, na ninatamani sana awe upande wetu. Kwangu ni muhimu sana nataka kujadiliana naye kwa undani zaidi kuhusu vita hivi."

Rais Volodymyr Zelensky akipeana mkono na Rais mteule wa Marekani Donald Trump walipokutana Septemba 27 huko New YorkPicha: Alex Kent/Getty Images

Trump anatarajiwa kuapishwa Januari 20 mwaka ujao na tayari ameahidi kuvimaliza vita hivyo mara moja.

Soma pia: Zelensky kuwasilisha "mpango wa ushindi" kwa EU na NATO

Kyiv na washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi kwamba Mrepublican huyo asiyetabirika huenda atasimamisha misaada ya kijeshi nchini Ukraine na kumlazimisha Zelensky kuingia kwenye makubaliano magumu na Urusi.

Lakini viongozi hao wamemuonya Trump kwamba hakutakuwa na jaribio litakalofanikiwa, ikiwa ataishinikiza Ukraine kuingia kwenye makubaliano huku Mkuu wa sera za kigeni Kaja Kallas akisema makubaliano ya lazima hayatakuwa na matokeo mazuri kwa Ukraine.

Zelensky asisitiza ushirikia wa Ulaya na Marekani

Lakini Zelensky amewasisitiza viongozi hao kwamba haitakuwa rahisi kuisaidia Ukraine wakiwa peke yao, bila ya kushirikisha Marekanina kuwaomba kushirikiana ili kumzuia Putin na kuiokoa Ukraine, ingawa alitahadharisha kwamba hatakubaliana na usitishwaji wa mapigano ambao utaipa nafasi Urusi kujipanga upya na kuwashambulia tena, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa na mpango madhubuti.

Baadhi ya wakuu wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wa kilele wa mwisho kwa mwaka 2024, mjini Brussels.Picha: Alexandros MICHAILIDIS/European Union

Kwenye mkutano huo Umoja huo umeahidi kutoa yuro bilioni 35 zaidi za msaada wa kifedha kwa ajili ya Ukraine ifikapo mwaka 2025, uliotangazwa na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa.

Suala la Syria pia lilijadiliwa

Ingawa vita vya Ukraine vilichukua nafasi kubwa, lakini suala la kuangushwa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad pia liligubika mkutano huo katikati ya wasiwasi juu ya mamlaka mpya inayoongozwa na kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), lililoorodheswa kuwa la kigaidi na baadhi ya serikali za Magharibi.

Nchi kama Italia inashinikiza kuchukuliwa hatua haraka huku Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo akisema Ulaya inatakiwa kuonyesha utayari wa kutoa msaada zaidi wa kibinadamu na kujaribu kuleta hali ya utulivu".

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amezungumzia kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi nchini humo, akisema hatua hiyo inatakiwa kuchukuliwa mara moja kwa kuwa maendeleo ya kiuchumi yana nafasi kubwa katika kipindi cha mpito baada ya utawala wa Assad.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW