1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walatino wamsaidia Trump kupata ushindi Florida

4 Novemba 2020

Wamarekani wenye asili ya Uhispania, Uholanzi au Brazil maarufu kama Walatino, wamemsaidia pakubwa Donald Trump kushinda jimbo la Florida. Ines Pohl anaandika kutoka Florida.

USA |Florida | Wahlen 2020 | Bertica Cabrera Morris
Picha: Ines Pohl/DW

Cabrera Morris ni mwanachama mashuhuri wa jamii ya Walatino katika jimbo la Florida, ambao wamemsaidia sana kumpa Donald Trump ushindi uliotarajiwa kwenye jimbo hilo muhimu. Pia alikuwa mshirika katika timu ya kampeni ya Donald Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Cabrera Morris ameishi nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 50. Alikimbia nchi yake ya Cuba alipokuwa na umri wa miaka 14. Amesema kuwa baba yake alilazimishwa kufanya kazi kambini nchini mwake kwa sababu hakutaka kuyakubali matakwa ya kisoshalisti mnamo mwaka 1967, miaka minane baada ya mapinduzi yaliyoongozwa na Fidel Castro. Mali ya kampuni za kimataifa na ya Wacuba matajiri ikanyakuliwa.

Soma zaidi: Rais wa Marekani ana nguvu kiasi gani?

Uchaguzi ulipokaribia, Cabrera Morris ambaye ni mfanyabiashara na pia mshauri wa kisiasa, alisema atafanya juu chini kuhakikisha Trump anasalia madarakani kwa muhula mwingine wa miaka minne, na kumzuia Joe Biden na Kamala Harris kuchukua urais na umakamu rais.

Cabrera Morris anakiri kuwa japo Biden na Harris si wasoshalisti, anaamini Wademokrat wengi wataipeleka nchi kufuata mkondo huo.

Makazi yake mazuri kabisa anayoishi pamoja na mumewePicha: Ines Pohl/DW

Wasiwasi wa Cabrera Morris unawahusu Wacuba wengi waliokimbia nchi yao kuingia Marekani baada ya mapinduzi. Awali Cabrera na mama yake walikimbilia Uhispania ambako mama yake alifanikiwa kuomba nafasi ya kuishi Marekani kihalali kupitia mpango wa Green Card. KWa hivyo anasema anaamini katika kile kijulikanacho kama ''Ndoto ya Marekani, maana walimpa hiyo ndoto''

Cabrera Morris anasisitiza kuwa yeye Pamoja na mama yake waliingia Marekani kwa njia halali. Haamini kwamba watu ambao wamefurushwa makwao katika mataifa ya Amerika ya Kusini mathalan Honduras au Guatemala, wanapaswa kuruhusiwa kuingia Marekani, hata kama wanaomba uhifadhi kwa sababu ya kuhofia maisha yao au mali yao. Anasema wanaweza kuwa mfano wa hoja hiyo na hawawezi kuwa walinzi wa dunia.

Anaupenda msimamo mkali wa Trump kuhusu wahamiaji. Aidha anapenda sera za Trump zinazowawezesha wajasiriamali kama yeye na mumewe kuendelea kunawiri. Hagutushwi na lugha ya Trump anayotumia mara kwa mara kuwaelezea jamii kutoka Amerika ya kusini. Amesema ikiwa Trump anawakosoa walanguzi wa mihadarati kutoka Mexico, haimaanishi anawakosoa Wamexico, anataka tu kuwakomesha wahalifu.

Soma zaidi:Unachopaswa kufahamu kuhusu uchaguzi wa Marekani

Usalama mipakani na ndani ya Marekani pia ni hoja muhimu kwa Cabrera Morris. Anamtizama Trump kuwa ndiye anafaa kuwa rais. Anawaunga maafisa wa polisi huku akiwalaumu wapinzani wa Trump kuhusu machafuko ambayo yameshuhudiwa katika maeneo kama Portland na Oregon ambako maafisa wa usalama walitumwa kuzima maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi katika asasi za nchi au katika maeneo ya Kenosha na Wisconsin ambako makundi yenye silaha yalikabiliana na waandamanaji waliopinga ukatili wa polisi, na mfuasi wa Trump kuwaua watu wawili mitaani.

Cabrera Morris anaipenda Marekani. Amesema aliyapigania na kufanya bidi ili kuyaishi maisha anayoyaishi sasa Pamoja na mama yake. Bustani yake ndogo iliyo na ndizi na maua ni kama paradiso ndogo kwake na humkumbusha Cuba.

(DW)

Mwandishi: Ines Pohl

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW