1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliberia wamchagua rais

Sekione Kitojo
26 Desemba 2017

Waliberia walipiga kura Jumanne kumchagua kiongozi wao kati ya mchezaji kandanda wa zamani wa kimataifa George Weah na makamu wa rais Joseph Boakai, katika uchaguzi ambao wachambuzi wanasema matokeo yatakaribiana

Liberia Wahlen
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Wagombea  hao  wawili  walijiunga  na  wapiga  kura  wengine  nchini  Liberia  leo  wakati wakipambana  katika  uchaguzi  huo   wa  rais ambao  ulicheleweshwa  wa  duru  ya  pili.

Wapiga  kura  wanamchagua  rais  ambaye  atachukua  nafasi  ya  rais  Ellen Johnson Sirleaf , ambaye  atajiuzulu  baada  ya  kutumia  miaka  12 kaka  rais  wa  kwanza  mwanamke katika  bara  la  Afrika , katika  mabadilishano  ya  kwanza  ya  madaraka  kidemokrasia katika  taifa  hilo  la  Afrika  magharibi  tangu  mwaka  1944.

Uchaguzi  huo ulicheleweshwa  kwa  wiki  saba  kutokana  na  kufikishwa  mahakama  kwa malalamiko yaliyotolewa  na  chama  cha  Boakai  cha  Unity dhidi  ya  tume  ya  uchaguzi kuhusiana  na  uendeshaji  wa  uchaguzi  wa  duru  ya  kwanza.

Weah  alikuwa  nyota  katika  timu  za  kandanda  barani  Ulaya  timu  kama  Paris Saint Germain  na  AC Milan   katika  miaka  ya  1990  kabla  ya  kucheza  kwa  muda  mfupi katika  klabu  ya  Chelsea   na  manchester  City  nchini  Uingereza  mwishoni  mwa  muda wake  wa  kucheza  kandanda.

Yee  na  Boakai  walipiga  kura  katika  vituo  vya  kupigia  kura  karibu  na  wanakoishi katika  eneo  la Paynesville, kitongoji  cha  mji  wa  Monrovia, mji  mkuu  wa  taifa  hilo  lenye wakaazi  milioni  4.6.

George Weah mchezaji wa zamani wa kandanda ambaye ni mgombea uraisPicha: picture-alliance/dpa/Pressefoto ULMER/M. Ulmer

Kila mmoja  atamba kuwa atashinda

Kila  mmoja  ametangaza   kwamba  ushindi  ni  wake  katika  kinyang'anyiro  hicho. "Tutashinda ! Kwasababu  watu  wanatuamini  na  wanajua  tunawakilisha  kilicho  bora," amesema  Boakai , mfanyakazi  wa  umma  kwa  muda  wa  miongo  minne, anayeonekana kwa  mgombea  wa  serikali.

Lakini  Weah  pia  nae  alionesha  matumaini  kwamba  kugombea  kwa  mara  ya  pili katika uchaguzi  wa  rais  mara  hii  kutakuwa  na  mafanikio.

"Ushindi  ni  hakika , nina  hakika  kwamba  nitashinda," aliwaambia  waandishi  habari baada  ya  kupiga  kura  yake.

Makamu wa rais wa Liberia Joseph BoakaiPicha: Imago/Xinhua

Weah  anadai  kwamba udanganyifu  katika  uchaguzi  ulimgharimu ushindi  mwaka  2005 na makamu  wa  rais  mwaka  2011. Chama  chake  cha  CDC kilipinga  matokeo  ya  uchaguzi wa  mwaka  2005  na  2011, lakini  kimejizuwia   hadi  sasa kufanya  hivyo  mwaka  huu.

Baada  ya  kupiga  kura   Jumanne (26.12.2017), Weah  alionya  kwamba "kile  kilichotokea mwaka  2005  na  2011 hakiwezi  kurejewa".

Boakai atoa  onyo

Boakai  pia  alitoa  onyo  kama  hilo, akisema atakubali  matokeo  iwapo tume  ya  taifa  ya uchaguzi "itatimiza  viwango  vyote".

Boakai alipambana  mahakamani kuhusiana  na  matatizo ya  udhibiti  wa  foleni  ya wapiga  kura  pamoja  na  utambulisho  wa  wapiga  kura  katika  uchaguzi  wa  Oktoba 10 wa  duru  ya  kwanza.

Katika  duru  ya  kwanza  ya  uchaguzi  Oktoba  10 , Weah  alipata  asilimia  38.4  ya  kura wakati  Boakai  alikuwa  wa  pili  akipata  asilimia  28.8  ya  kura. Hali  hiyo  ilisababisha kufanyika  duru  ya  pili  ya  uchaguzi  kwa  kuwa  hakuna  mgombea  aliyeweza  kuvuka asilimia  50 ya  kura  inayohitajika  kushinda  uchaguzi  moja  kwa  moja.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Isacc Gamba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW